Mbio kubwa za Ruaha kuanza Julai 4

DAR ES SALAAM: Kadri siku zinavyosogea kuelekea mwezi Julai, macho ya Watanzania na dunia yanaelekezwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambako pazia la mbio za mbio kubwa za Ruaha maarufu ‘Great Ruaha Marathon’ zitakazofanyika Julai 4, 2026 litafunguliwa Julai 3, 2026 kwa utulivu wa asili kupitia walking safari na spot fishing.

Great Ruaha Marathon si tukio la kawaida la michezo bali imekuwa simulizi ya nchi inayoandikwa kwa hatua za wakimbiaji, katikati ya mandhari ya pori hai, ambapo sauti za upepo, ndege na wanyamapori zinakuwa sehemu ya mashindano.

Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, washiriki hawakimbii tu kushindan wanakimbia wakigusa uzuri wa asili ambao nchi nyingi zimekuwa zikiutafuta.

Uzinduzi rasmi wa usajili wa msimu wa tano umefanyika jijini Dar es Salaam, ukiweka wazi dhamira ya kulifanya tukio hili kuwa daraja la kuunganisha michezo, utalii, afya na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Msajili wa Hazina na mlezi wa marathon hiyo, Neemia Mchechu, alisema tukio hilo lina nafasi muhimu katika kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania duniani.

“Ni tukio adimu. Ni nadra kuona binadamu na wanyamapori wakishiriki anga moja kwa amani ndani ya mazingira ya asili. Hii ni fursa ya kuitangaza Tanzania kwa dunia,” alisema Mchechu.

Alisisitiza kuwa ukuaji wa sekta ya utalii nchini unaendelea kushika kasi, akitolea mfano ongezeko la watalii mwaka hadi mwaka, huku akihimiza juhudi zaidi kuelekezwa kusini mwa Tanzania ambako kuna hazina kubwa ya vivutio.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika linaloandaa marathon hiyo, Eward Athanas, alisema maandalizi ya mwaka huu yameboreshwa kwa kiwango kinachoendana na matarajio ya washiriki wa ndani na kimataifa.

“Hii siyo marathon ya kawaida. Tunazungumzia tukio linalounganisha michezo, utalii na uhifadhi kwa wakati mmoja. Mwitikio kutoka Ulaya na Amerika utakuwa mkubwa, na hilo linatupa picha kuwa Ruaha Marathon sasa inaingia kwenye jukwaa la kimataifa,” alisema Athanas.

Aliongeza kuwa GRUMA imejikita katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, hasa kulinda mfumo wa ikolojia wa Mto Ruaha Mkuu, huku pia ikitoa nafasi kwa vijana kushiriki katika maendeleo kupitia michezo na utalii endelevu.

“GRUMA ni zaidi ya mbio; ni jukwaa la elimu, afya na maendeleo. Tunataka kila mshiriki aondoke hapa akiwa na uzoefu wa kipekee na uelewa mpana wa umuhimu wa kulinda mazingira,” alisisitiza.

Mratibu wa mbio hizo, Hamim Kilahama, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kusisitiza upekee wa tukio hilo kufanyika ndani ya hifadhi ya taifa—jambo linalolifanya kuwa miongoni mwa matukio machache duniani yanayowezesha watu kukimbia katikati ya wanyamapori.

Mbali na mbio za kilomita tano, 10 na 21, pamoja na mashindano ya baiskeli ya kwanza ya baiskeli, washiriki pia watapata fursa ya kushiriki katika shughuli nyingine za utalii ikiwemo ziara ya kuangalia wanyama, uvuvi wa michezo na matembezi ya asili mchanganyiko utakaolifanya tukio hili kuwa zaidi ya mashindano ya riadha.

Alisema kwa wadau wa uchumi na utalii, GRUMA imeanza kuonekana kama kichocheo kipya cha maendeleo ya kusini mwa Tanzania.

Kupitia ongezeko la washiriki kila mwaka, tukio hili linafungua milango ya ajira, biashara ndogo ndogo na uwekezaji katika sekta ya huduma.

Usajili wa kushiriki tayari umefunguliwa rasmi, huku waandaaji wakihimiza watanzania na wageni kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo sio tu kwa ajili ya ushindani, bali kwa ajili ya kuwa sehemu ya uzoefu wa kipekee unaoitangaza Tanzania na vivutio vyake kwenye ramani ya dunia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button