Mbio za nyika Taifa ziwe na ushindani

UONGOZI wa Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT) umesema kuwa mwaka huu hakutakuwa na mashindano ya taifa ya riadha, kwa sababu muda hautoshi.

Viongozi wa shirikisho hilo wanasema kuwa tangu waingie madarakani Agosti mwaka huu, wamekuwa na muda mfupi wa kuandaa mashindano hayo.

Badala yake, viongozi hao wametangaza Novemba 15, 2025 kuwa kutakuwa na mashindano ya taifa ya Mbio za Nyika yatakayofanyika mkoani Arusha na yatakuwa ya wazi ambapo kila mkoa unatakiwa kushiriki.

SOMA: Mbio Mount Meru kufanyika Novemba 3

Ni matarajio ya wadau wengi wa mchezo huo kwamba badala ya kuwa na mashindano ya taifa ya riadha, basi kuwe na mashindano mazuri ya nyika na yatakayoshirikisha mikoa karibu yote.

Mara nyingi tumeona mikoa ikikacha kuleta timu zao katika mashindano ya taifa na kusababisha mashin- dano hayo kukosa msisimko wa aina yake unaotarajiwa kuwepo.

SRT ndiyo yenye jukumu la kuendeleza mchezo huo kitaifa, huku likigawa madaraka kwa mikoa kutekeleza mpango huo katika wilaya, ikiwa pamoja na kuhakikisha wanafanya mikutano na mashindano ya wilaya.

Viongozi wa SRT waliopo sasa madarakani, wanapaswa kutekeleza jukumu hilo ambalo lipo kikatiba.

Inashangaza kuwapo mikoa ambayo haipeleki timu zao katika mashindano ya taifa lakini imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika uchaguzi wa kitaifa wa shirikisho hilo.

Isije ikawa ni kwa sababu wanalipiwa gharama za malazi, chakula na posho wakati katika mashindano, mara nyingi hivyo vitu havitolewi.

Ni matarajio yetu kuwa pamoja na kutoandaa mashindano ya taifa mwaka huu, mashindano hayo yatakuwa ya aina yake na mikoa itaandaa timu zao kutoa ushindani mkubwa si tu kushiriki, bali pia kuongeza idadi.

Viongozi wanaoshindwa kuendeleza mchezo huo katika maeneo yao husika hawafai kuendelea kuwepo, hasa hao wa mikoa na wilaya.

Kwa sababu hiyo, SRT wanatakiwa kuiangalia mikoa kama inaleta maendeleo ya mchezo huo na kufanya mi- kutano, ikiwemo ule wa uchaguzi muda unapofika. Pia, wanatakiwa kuichunga wilaya na mikoa kuhakikisha inafanya mikutano na mashindano.

Kama kila mtu angewajibika katika sehemu yake kwa mujibu wa katiba iliyomuweka madarakani, riadha ingeenda juu kwa haraka.

Viongozi wa kitaifa wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuanzia kuwabana viongozi wa mikoa katika mashindano hayo ya taifa ya Mbio za Nyika

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button