Mbio Mount Meru kufanyika Novemba 3

MBIO za Mount Meru zilizokuwa mbio za riadha jijini Arusha kwa miaka ya nyuma sasa zimerejea upya na zinatarajiwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu.

Dinnah Mosha mwandaaji wa mbizo hizo amesema mbio hizo ni kongwe zilizovuma kawa muda mrefu lakini sasa zimerejea ikihusisha kilomita 21, kilometa 10, kilometa 5 na kilometa 2.5 kwa watoto ambapo zitaanzia uwanja wa General Tyre na kumalizikia hapo.

Amesema lengo kuu la Mount Meru Marathoni ni kukuza utalii huku ikiwa Arusha ni jiji la kitalii, kuimarisha afya kwa maana ya mazoezi  na pia kumjenga mtoto wa kiume kwa maana ya kusimamia  malezi yake kiujumla na kuwa nao karibu kama ilivyo kwa mtoto wa kike.

Advertisement

“Nawashukuru wadhamini wote waliotuunga mkono na kuwa sehemu ya kufanikisha mbio hizi,”amesema Mosha.

Akizungumza kuelekea mbio hizo, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema mbio hizo zinabeba utambulisho muhimu kwa Arusha kwa sababu Mlima Meru ni kilele cha pili kwa urefu nchini na kushika nafasi ya tisa katika Bara la Afrika hivyo ni kivutio cha utalii.

“Tunapoona wadau kama hawa wanaanzisha matukio haya tunakuwa  sehemu ya kuwaunga mkono  na katika hilo pia mimi nitashiriki  mbio za Mount Meru Marathon 2024 mimi na familia yangu lengo ni kuunga mkono juhudi hizi za kuinua na kuhamasiha michezo na utalii,” amesema Gambo.

Amesema pia mbio hizo zitachangia kuchochea hali ya kiuchumi jijini Arusha.

“Nimefurahi kuona watoto watakuwa sehemu ya ushiriki na mimi nitaleta watoto wangu waungane na wenzao katika jambo hilo kubwa,”ameeleza  Gambo.

Gambo alimshukuru Rais  Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuunga mkono kwenye masuala ya michezo,Afya na Utalii  na kusema amefarijika kusikia kutoka kwa waandaaji kuwa baada ya mbio kitakachopatikana kitarudishwa katika jamii kusaidia wenye uhitaji wanaosumbuliwa na magoinjwa mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Arusha (ARAA) Gerald Babu amesema wanashirikiana kwa  ukaribu na waandaaji ili kuweza kuhakikisha mbio zinafanikiwa kwa misingi ile ile na malengo yaliyokusudiwa.