Mkakati waiva kukuza vipaji UMITASHUMTA, UMISETA

IRINGA: SERIKALI imetangaza mkakati mpya wa kitaifa wa kutambua, kusajili na kufuatilia vipaji vinavyoibuliwa kupitia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA, hatua inayolenga kuhakikisha hakuna kipaji kinachopotea na kwamba vijana wenye uwezo katika michezo na sanaa wanapata nafasi ya kuendelezwa hadi kufikia ngazi za kitaifa na kimataifa.

Sambamba na hilo, serikali imeelekeza halmashauri zote nchini kuanzisha shule maalumu za kukuza vipaji na kutenga fedha za maendeleo ya michezo na sanaa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya ajira, afya bora na maendeleo ya uchumi.

Mkakati huo umetangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof Riziki Shemdoe, wakati akizindua rasmi Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) Kitaifa 2026 yanayofanyika katika viwanja mbalimbali vya mjini Iringa.

Prof Shemdoe, aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, amesema michezo na sanaa zimekuwa sekta muhimu zinazoweza kuibua vipaji, kuzalisha ajira na kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Aleema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Michezo na Sanaa Shuleni; Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa” inaakisi dhamira ya serikali ya kutumia michezo na sanaa kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Mashindano haya si kwa ajili ya medali na vikombe pekee. Hapa tunajenga kizazi cha vijana wenye nidhamu, uzalendo, kujiamini na uwezo wa kushindana katika viwango vya juu zaidi,” alisema Prof Shemdoe.

Alibainisha kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya michezo shuleni, kuimarisha uratibu wa michezo na sanaa pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika vituo vya kukuza vipaji na akademia za michezo nchini.

Aidha, alizitaka halmashauri zote kulinda maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za michezo na kuhakikisha vipaji vinavyogunduliwa vinapata mazingira rafiki ya kukuzwa na kuendelezwa.

Prof Shemdoe alisema dunia ya sasa imeifanya michezo na sanaa kuwa taaluma inayoweza kubadili maisha ya vijana wengi, hivyo kuna umuhimu wa Tanzania kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ili kuzalisha wanamichezo na wasanii wenye uwezo wa kushindana katika majukwaa ya kimataifa.

Mashindano ya mwaka huu yamewakutanisha zaidi ya washiriki 9,600 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Takwimu zinaonyesha kuwa UMITASHUMTA imehusisha wanafunzi 3,417 wa shule za msingi pamoja na walimu 905, huku UMISETA ikiwakutanisha zaidi ya wanafunzi 3,400 wa shule za sekondari pamoja na walimu, makocha na viongozi wa michezo wapatao 900.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira salama na yenye ushindani wa haki.

Alisema Iringa imeendelea kuaminiwa kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kitaifa kutokana na uwezo wake wa maandalizi na miundombinu inayokidhi mahitaji ya mashindano makubwa.

“Mkoa wetu umejipanga vizuri. Vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini kuhakikisha washiriki wote wanakuwa salama wakati wote wa mashindano haya,” alisema Kheri.

Aliwataka wananchi wa Iringa kuendelea kuonyesha ukarimu kwa wageni waliotoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwahimiza wafanyabiashara kutoa huduma bora zitakazoendana na hadhi ya mashindano hayo.

Mbali na ushindani wa michezo na sanaa, UMITASHUMTA na UMISETA vinaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vipya vinavyoweza kuzaa nyota wa baadaye wa Tanzania katika soka, riadha, mpira wa kikapu, netiboli, sanaa za maonesho na michezo mingine.

Kadri mashindano hayo yanavyoendelea mkoani Iringa, matumaini ya taifa yanaendelea kuelekezwa kwa maelfu ya vijana wanaoshiriki, huku serikali ikiamini kuwa baadhi yao watakuwa mabingwa, wasanii na mabalozi wa Tanzania katika miaka ijayo.

Kwa wengi, UMITASHUMTA na UMISETA si mashindano ya kawaida bali ni kiwanda cha vipaji, shule ya uongozi na daraja la ajira kwa kizazi kijacho cha Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button