Mbowe aomba nyufa, mifarakano Chadema kuzibwa

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe amewataka viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa chama hicho kuziba nyufa na mifarakano ndani ya chama hicho kuendelea kukiimarisha.

Awali, Mbowe alisema chama hicho kimepita kwenye milima na mabonde kwa miaka saba lakini hakikutetereka, bali kilisimama na kuwa bora.

Aliyasema hayo jana Dar es Salaam akihutubia Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee la Chadema (BAZECHA).

“Uvumilivu wetu ndio umetufanya tusimame hadi leo kwani tuna uwezo wa kufanya mikutano nchi nzima na watu wakajaa. Wito wangu kwenu ninyi mtakaochaguliwa hakikisheni mnakwenda kusimamia chama, kuziba nyufa na mifarakano ndani ya chama,” alisema Mbowe.

Aliwataka wazee hao kujiimarisha na kukiandaa chama kuelekea uchaguzi wa baadaye mwaka huu.

Alisema kumekuwepo na minyukano inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii inayolenga kukiangusha chama hivyo kuwataka wazee hao kumpinga shetani na mambo yake yote.

“Katika hayo yanayoendelea tuna mambo ya kujifunza ambayo ni kutambua kuwa chama hiki ni bora na kikubwa kuliko yeyote,” alisema Mbowe.

Alisema milango iko wazi kwa yeyote mwenye kutaka kuleta mabadiliko na hakuna wa kuleta ugomvi, bali ni wakati wa kushirikiana na kushauriana namna nzuri ya kuleta maendeleo ndani ya chama.

Aliwaonya vijana kuhukumu na kuita wazee kuwa ni laana ndani ya chama, bali watambue nafasi na michango ya watu hao kwani busara zao ndizo huendelea kukikuza chama.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu aliwatakia Bazecha uchaguzi mwema na kuwahimiza kuchagua viongozi bora watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Aidha, Katibu Mkuu wa chama, John Mnyika alitangaza Kamati ya Wazee wastaafu wanane watakaosimamia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 21, mwaka huu.

Mnyika aliwataja wazee hao ni Alfred Kinyondo, Ahmed Rashid, Profesa Azaveli Lwaitama, Wakili Edson Mbogoro, Francis Mushi, Lumuli Kasyupa, Profesa Raymond Mosha na Ruth Mollel.

Mnyika alisema uteuzi huo umefanywa na Kamati Kuu katika kikao cha Januari 11, mwaka huu.

“Uteuzi wa wazee wastaafu hawa umefanywa na Kamati Kuu katika kikao chake cha tarehe 11 Januari 2025 kwa kuzingatia Kanuni za chama Kifungu cha 7.3 juu ya Taratibu za Kusimamia Chaguzi na kupiga kura Kipengele cha 7.3.1,” alieleza Mnyika.

Katika uchaguzi wa jana, jumla ya wajumbe walitarajiwa kuamua yupi awaongoze kati ya wagombea 88 wanaowania nafasi ya uenyekiti nafasi tano, Makamu Mwenyekiti Bara mmoja, Makamu Mwenyekiti Zanzibar wagombea wawili, Katibu Mkuu wagombea watatu, Naibu Katibu Mkuu Bara wawili, na Zanzibar mgombea mmoja.

Nafasi nyingine ni Mweka Hazina mgombea mmoja, wajumbe wa Baraza Kuu wagombea 23 kati yao wawili kutoka Zanzibar, na wajumbe wa Mkutano Mkuu wagombea 48 kati yao watano kutoka Zanzibar.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana (BAVICHA) Taifa utakaowachagua viongozi mbalimbali, Mbowe amesema kutukanana na kudhalilishana si sehemu ya kujenga chama imara na kuwataka vijana kusimamia nidhamu na kupendana.

“Wengi wenu mmezaliwa mmekikuta chama hiki kwa sababu watangulizi wenu waliheshimiana, walipendana, walipatana, na wakawiwa pamoja na kufanya kazi pamoja kukijenga chama, lakini tabia iliyojionesha kwenye uchaguzi wa mwaka huu sio utamaduni wa chama,” alisema Mbowe.

Aidha, Mbowe amewataka uongozi mpya wa Bavicha kufanya kazi ya kukiunganisha chama katika ngazi ya chini.

Mbowe pia amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 wasitegemee urahisi hivyo baraza hilo liandae mikakati na mipango endelevu kuimarisha chama chao.

“Wale ambao watachaguliwa kwenye chama au mabaraza ya chama wakafanye mambo makubwa ya kuongeza nguvu kuhuisha chama katika vitongoji,” alisema Mbowe.

Naye Lissu amelitaka baraza hilo kutambua wajibu wa vijana katika kujenga nchi.

Mwenyekiti wa Bavicha anayemaliza muda wake, John Pambalu amehimiza uchaguzi wa huru na haki akiwataka wajumbe kuchagua viongozi kwa sifa, uwezo na ubora.

Mkutano huo umewakutanisha wajumbe zaidi ya 320 kutoka katika kanda mbalimbali.

 

Habari Zifananazo

Back to top button