Mbowe: Sijatimiza maono kuijenga Chadema

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema sababu ya yeye kugombea tena nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho ni kuendeleza mapambano ili kutimiza maono waliyonayo yeye na wapambanaji wengine kwa chama hicho.

Aliyasema hayo jana alipozungumza katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds cha Dar es Salaam kujibu swali la kwa nini asitumie busara kuachia madaraka kwa kuwa amekaa muda mrefu kwenye nafasi hiyo na kwamba watu wameanza kumchoka.

Mbowe amekaa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema kwa miaka 21 tangu alipochukua nafasi hiyo mwaka 2004 kutoka kwa Bob Makani ambaye alikiongoza chama hicho kwa miaka minne tangu mwaka 1999.

“Kwenye vyama vya siasa vya upinzani kuwapata watu wenye maono si kazi nyepesi kwa sababu watu wanakimbia wajibu huu, pili tuna maono tunayopigania hatujayafikia na bado kuna kazi kubwa, mimi kama mmoja wa wasisi wa chama hiki naona tumepiga hatua kubwa lakini bado hatujafikia malengo yetu, kwa hiyo bado si kipindi cha kupunguza nguvu wala kuchukua likizo, ni kipindi cha kuongeza nguvu.

“Mimi sijawahi kujichagua lakini unaangalia, nawaacha wenzangu wanaopigana! Kazi ya upinzani ni vita! Hakuna majenerali wanakimbia vita wakasema ni majenerali, wanapigana mpaka ama wafie kwenye uwanja wa vita, au wapate kile ambacho walikuwa wanakipigania,” aliongeza.

Alisema hakuna mtu anayekatazwa kugombea nafasi yoyote ndani ya Chadema, wanachama ndiyo wenye mamlaka ya kuamua na anaamini iko siku zama zake zitafika mwisho hata kama bado anazo ndoto

Alisema kila binadamu ana ndoto zinazopaswa kuheshimiwa na kuongeza kuwa kauli ya wengi ni lazima iheshimiwe na wala si kwamba Chadema hakuna ukomo wa madaraka kwa kuwa wako watu ambao watakoma madaraka kwenye uchaguzi wa mwaka huu ama kwa kutokugombea kwa hiyari, au kwa kutoteuliwa katika hatua za awali.

Alisema ili kujenga heshima ya taasisi na viongozi ni lazima kufata taratibu zilizowekwa katika kubadilisha uongozi badala ya kutumia propaganda zinazochafua chama.

Kuhusu mabadiliko ya katiba, Mbowe alisema katiba ya Chadema imeweka wazi utaratibu na mchakato wa kufanya mabadiliko na kila mwanachama bila kujali nafasi yake ya uongozi ana uhuru wa kupendekeza mabadiliko lakini mpaka sasa hakuna mwanachama aliyejitokeza kufanya hivyo.

Alisema anashangaa na kujiuliza wale wanaotoa msukumo wa yeye kuondoka kwamba ni wale aliokaa nao kwa kipindi kirefu madarakani wakifanya kila uamuzi wa chama pamoja na kwa kukubaliana lakini leo wanathubutu kutoa siri za chama na hata kukibagaza kuwa kuna rushwa ndani yake.

Kuhusu hoja kwamba alichukua rushwa wakati alipokwenda kuzungumza na Rais kuhusu maridhiano, alisema hakuwahi kupokea chochote na kwamba kila hatua iliyofanyika kwenye maridhiano hayo ikiwa ni pamoja na kuandaa hoja 11 zilizopelekwa kwenye meza ya maridhiano, ilifanywa kwa ushirikiano na viongozi na Kamati Kuu ya Chadema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button