MBUNGE wa Jimbo la Ulanga mkoani Morogoro, Salim Alaudin Hasham, amesema hatamfumbia macho mtu yeyote atakayekwamisha mradi wowote unaosimamiwa kupitia fedha za mfuko wa jimbo.
Mbunge Salim ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara Uwanja wa Shule ya sekondari mwaya Kata ya Ruaha kwa lengo la kuwaomba wananchi kujitolea kweny ujenzi wa miradi mbalimbali, ili iweze kukamilika kwa wakati na ianze kutoa huduma.
Mbunge Salim pia amesema kwa mwaka 2022/2023, Jimbo la Ulanga limepata kiasi cha Sh 89,140,000 za mfuko wa jimbo, ikiwa ni fedha nyingi kupatiwa tangu aingie madarakani.
Amesema kiasi cha Sh Mil 50 amekielekeza kukamilisha bweni la wasichana Shule ya sekondari Mwaya Kata ya Ruaha kwa lengo la kupunguza mimba za utotoni na kuinua kiwango cha elimu katika hilo.
Pia Mbunge Salim amemtaka mhandisi wa halmashauri hiyo, Amir Athumani kuhakikisha wanazitumia vyema fedha hizo na zinakamilisha mradi huo wa bweni kwa wakati bila kikwazo chochote, ili watoto wa kike waanze kulitumia.
Mbali na mkutano huo, Mbuge Salim pia amefanya ziara ya kukagua miradi yote iliyopata fedha za mfuko wa jimbo kwa mwaka 2021/22, ili kujiridhisha kama fedha hizo zimefanya kazi vyema kama ilivyoelekezwa na kamati ya mfuko wa jimbo katika vikao vyao.
Amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuikumbuka Wilaya ya Ulanga katika nyanja mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo.