Mchengerwa atoa siku 27 watumishi wapya kulipwa fedha za kujikimu

DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ametoa siku 27 kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanalipa fedha za kujikimu kwa Watumishi wa ajira mpya za Ualimu na Afya.
Mchengerwa amesema watumishi wa ajira mpya za uwalimu na afya walioripoti vituo vyakazi kuanzia mwezi Julai, 2023 walipwe fedha zao za kujikimu kabla ya Oktoba 30, 2023.
Taarifa ya Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini imesema kuwa Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Oktoba 3, 2023 na kudai kuwa tayari serikali imeshapeleka fedha kwenye kila Halmashauri kwa ajili ya kulipa stahiki za watumishi hao.
“Serikali ilishapeleka fedha katika kila halmashauri lakini inashangaza mpaka leo kuna watumishi wa ajira mpya hawajalipwa fedha za kujikimu, hii sio sawa kwa watumishi,”amesema na kuongeza
“Fedha za kujikimu ni haki ya kila mwajiriwa mpya sasa, kwanini usilipe na fedha unayo kama kuna changamoto yeyote iwasilishwe ila sio kukaa na fedha na kuacha hawa watumishi wakihangaika, walipwe mara moja.”amesisitiza Mchengerwa.
Kwa mwaka wa fedha 2022/23, Serikali iliajiri watumishi wapya wa kada ya Ualimu na Afya ambapo kwa Kada ya Ualimu ni watumishi 13,130 na Afya ni watumishi 7,192 na wote wamekwisharipoti kwenye vituo vyao vya kazi.



