MCT kumpa tuzo Nyerere ukombozi, uhifadhi

BARAZA la Habari Tanzania (MCT) litamtunuku Baba wa Taifa, Julius Nyerere tuzo maalumu ya miaka 30 ya baraza hilo kutambua mchango wake wa kuweka misingi ya kutumia vyombo vya habari kukomboa nchi za Kusini mwa Afrika.
Tuzo hizo zitatolewa katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC) na MCT inaeleza kuwa misingi hiyo iliwapa nguvu wapigania uhuru kuwasiliana kwa ufanisi na hatimaye kufanikisha harakati za kujikomboa.
Baraza hilo linaeleza kuwa Nyerere alipigania kuanzishwa vituo vya taifa vya utangazaji katika nchi za Afrika ikiwemo Zimbabwe, Namibia, Botswana, Zambia na nyinginezo ili kuhakikisha vyombo vya habari vinatumika kuelimisha, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda maadili ya Kiafrika.
“Mkakati huu ulikuwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha Waafrika kurejesha simulizi zao, historia yao, urithi wao na hatima yao mikononi mwao,” ilieleza MCT.
Iliongeza: “Tunamtambua rasmi na tunataka kumtunuku Mwalimu Julius Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa wa kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, kujenga amani na mshikamano wa bara na kukuza demokrasia”.
MCT ilieleza kuwa tuzo hiyo inatolewa kwa ushirikiano wa Azam Group na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kuzingatia kuwa mnamo mwaka 1961 Nyerere alitoa Tamko la Uhifadhi la Arusha.
Baraza hilo lilinukuu maneno ya Baba wa Taifa akisema, “Uhai wa wanyamapori wetu ni suala muhimu sana kwa watu wote wa Afrika… tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu wa watoto wetu watafurahia urithi huu adhimu na wa thamani kubwa.”
Kwa mujibu wa MCT wakati wa uongozi wa Nyerere zaidi ya asilimia 28 ya ardhi ya Tanzania ilitengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.
“Sera zake ziliwezesha kuishi kwa amani kati ya wanyamapori na jamii ya Kimasai, hivyo kuhifadhi pamoja urithi wa kitamaduni na bioanuwai. Mwalimu Nyerere anahesabiwa kuwa Mhifadhi wa Kwanza wa taifa,” imeeleza MCT.
Baraza hilo limependekeza tuzo hiyo kwa Baba wa Taifa ianzishe tuzo za hifadhi za wanyamapori za Nyerere zitakazotumika kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika na duniani kote.