Menejimenti ya Maafa na umuhimu utabiri wa hali ya hewa

HIVI karibuni, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mvua za msimu wa vuli ambazo kwa kawaida huanza Oktoba hadi Desemba.

Akitoa utabiri huo, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a anabainisha uwepo wa mvua za wastani hadi chini ya wastani kwa maeneo mengi yanayopokea mvua za vuli na mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo machache.

Aidha, TMA inabainisha kuwa, msimu wa vuli utaambatana na kipindi cha joto kali kwa maeneo mengi. Inatoa angalizo la kutokea kwa matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo vipindi vya mvua kubwa hata kwa baadhi ya maeneo yanayotabiriwa kuwa mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Mbali na kutoa utabiri huo, Dk Chang’a pia anaeleza athari za kisekta zinazotarajiwa kutokea sambamba na kushauri namna ya kukabiliana na madhara au matokeo tarajiwa katika msimu huo. Kupitia utabiri huo, wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

SOMA: TMA yakabidhiwa rada mbili

Kilimo na usalama wa chakula Kupitia ushauri huo wa TMA, Dk Chang’a anasema maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani yanaweza kukumbwa na upungufu wa unyevu, unaoweza kuathiri ukuaji wa mimea na kusababisha upungufu wa mavuno hususani kwa mazao yanayotegemea mvua.

Aidha, kuna uwezekano wa ongezeko la wadudu na wanyama waharibifu kama mchwa na panya. Kwa hali hiyo, wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, sambamba na kutumia teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani.

Mengine ni kuzuia mmomonyoko na upotevu wa rutuba kutokana na kutuamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko na hata kuhifadhi maji shambani kwenye maeneo yanayotarajiwa kupata upungufu wa mvua. Mifugo na uvuvi Pia, utabiri huo unabainisha kuwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa maji unaweza kujitokeza.

Kwamba, hali hiyo inaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na pengine kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, jambo linalopaswa kuepukwa. Vilevile, katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo pamoja na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza. TMA inawashauri wafugaji kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo, ili kukabiliana na athari zitakazojitokeza.

Utalii na Wanyamapori Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinazotarajiwa zinaweza kusababisha uhaba wa malisho na maji kwa wanyamapori katika mbuga na mapori ya akiba na hivyo kusababisha migongano ya wanyamapori na jamii inayowazunguka.

Hata hivyo, habari zinabainisha kuwa mvua nyingi zinaweza kusababisha kutuama na kusambaa kwa maji na kusababisha kuhama kwa wanyamapori, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Hayo ni sambamba na maambukizi ya magonjwa ya wanyama wafugwao kutoka kwa wanyamapori wanaoingia kwenye makazi ya watu. Kutokana na utabiri huo, mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu mbalimbali katika mbuga na mapori ya akiba na kujenga uelewa kwa jamii, ili kuchukua hatua stahiki dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Idara ya Menejimenti ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni moja ya wadau wa kisekta wanaonufaika na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinaotolewa na TMA.

Taarifa ya idara hiyo iliyotolewa kwa gazeti la HabariLEO mwanzoni mwa wiki inabainisha kuwa, utabiri wa vuli unaotolewa ni nyenzo muhimu kwa Idara ya Menejimenti ya Maafa katika kutekeleza majukumu yake ya kuratibu shughuli za kuzuia na kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa (kama yatatokea).

Taarifa hiyo inasema kupitia taarifa za hali ya hewa, idara hupata mwongozo wa kitaalamu unaowawezesha wadau kuchukua hatua za mapema na zenye tija. Anasema kwa msingi huo, utabiri huo unafanikisha idara kuzielekeza kamati za usimamizi wa maafa za ngazi zote mikoa mpaka vijiji kuchukua hatua.

Hatua hizo zinalenga kupunguza athari za maafa katika maeneo yaliyo katika hali hatarishi. Taarifa inasema utabiri huo unasaidia kuwezesha utambuzi na tathmini ya maeneo hatarishi, hivyo kuruhusu tathmini ya kina na uwekaji wa vipaumbele katika mipango ya kujiandaa na kukabiliana na athari tarajiwa.

“Taarifa ya utabiri inawezesha maandalizi ya upatikanaji na uhifadhi wa vifaa vya msaada wa kibinadamu katika maghala,” inasema sehemu ya taarifa hiyo. Anaongeza: “…Pamoja na maandalizi ya rasilimali watu, fedha, vifaa pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbegu zinazokomaa muda mfupi na uhifadhi wa chakula cha dharura kwa binadamu na mifugo.”

Sambamba na hayo, idara inaweka mkakati wa kujenga uelewa na utayari kwa jamii kuhusu namna ya kujiandaa mapema, jambo linaloongeza uimara na ustahimilivu wa kijamii. Pia, Idara ya Menejimenti ya Maafa hutumia utabiri huo kutoa taarifa na miongozo kwa sekta mbalimbali kuchukua hatua mahususi kupitia vyombo vya habari.

Sekta hizo ni pamoja na kilimo na mifugo, ambapo wanaelekezwa kutumia mvua kwa manufaa ya maendeleo ya kilimo kwa kulima mazao yanayohitaji maji mengi kama mpunga au mazao yanayohitaji maji kidogo kama mihogo na mtama kadiri ya taarifa za utabiri za eneo husika.

Kuhusu mifugo na uvuvi, wahusika wanashauriwa kujenga miundombinu ya kuvuna maji, sambamba na kufanya maandalizi ya malisho na nyasi za akiba. Kwa upande wa sekta ya afya, idara inaelekeza kuweka mipango madhubuti ya kudhibiti milipuko ya magonjwa ya binadamu na mifugo yanayoweza kuzuka.

Sekta ya nishati nayo haiachwi nyuma. Inaelekezwa kupanga mikakati mapema kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kushughulikia changamoto za upatikanaji wa nishati zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya mvua.

Uhifadhi wa wanyamapori unaelekezwa kuimarisha ulinzi na udhibiti wa maeneo ya hifadhi ili kupunguza mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori. Hii ni kwa kuwa mwingiliano huo unaweza kuongezeka kutokana na uhaba wa rasilimali maji baina ya makazi ya watu na ya wanyamapori.

Kutokana na utabiri wa msimu ujao wa mvua za vuli, Idara ya Menejimenti ya Maafa inasema imejiandaa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kushirikiana na sekta na wadau husika kupanga mipango na kuchukua hatua za tahadhari ya awali.

Hii inalenga kujiandaa, kuzuia na hata kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika maeneo yaliyotabiriwa kuathirika. Nyingine ni kuelekeza kamati za usimamizi wa maafa kufanyia kazi taarifa za tahadhari za mapema kwa mikoa na wilaya zilizotabiriwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani zenye uwezekano mkubwa wa kupata mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Sambamba na hayo, kuratibu maandalizi ya mpango wa dharura utakaohusisha sekta zote muhimu. Hizo ni pamoja na sekta za kilimo, mifugo, maji, afya, nishati, miundombinu pamoja na wadau wa maendeleo na asasi za kiraia kuimarisha uwezo wa kujiandaa na kukabiliana haraka endapo maafa yatatokea.

Hatua nyingine ni kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabili, ikiwemo kuepuka kuishi katika maeneo hatarishi ya mito na mabonde, kufuata ushauri wa kitaalamu pamoja na kujikinga dhidi ya magonjwa ya milipuko.

Aidha, idara inajiandaa kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa kuandaa na kuweka akiba ya chakula cha msaada.

Vingine vya kuandaa ni vifaa vya uokoaji, utoaji huduma za afya na kijamii (yakiwamo mahema na dawa), kuboresha mifumo ya mawasiliano pamoja na uratibu ili kuimarisha hatua za kukabiliana na dharura, hasa katika maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuathirika vibaya kwa mvua za vuli.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button