MWILI wa mfamasia wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke, Magdalena Kaduma umekutwa umefukiwa pembezoni mwa nyumba aliyokuwa akiishi huku sababu ya kifo chake ikiwa haijulikani na mume akishikiliwa na polisi.
Inadaiwa kuwa tangu alipoondoka nyumbani kwake Desemba 4, mwaka huu kuelekea kazini kwake, hakuonekana nyumbani hadi juzi saa 9:00 alasiri ndugu zake na wajumbe wa Mtaa Hondogo, Kata ya Kibamba, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam walipobaini mwili wake ukiwa umefukiwa meta 15 kutoka ilipo nyumba yake.
Mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa wa Hondogo, Leonard Sabuni, walisema kuwa walikuta mwili huo ukiwa umevimba na kuanza kutoa harufu.
Katika tukio hilo, mume wa Magdalena ambaye hajafahamika jina, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kutokana na kifo hicho huku mfanyakazi wa ndani wa kiume aliyekuwa akiishi pamoja nao, akidaiwa kuwa ametoroka.
Akizungumza na HabariLEO kuhusu tukio hilo jana, Sabuni alisema kuwa juzi (Ijumaa) saa 4:00 asubuhi, wazazi wa Magdalena wanaoishi Tabata ulipo msiba kwa sasa, walifika ofisi za mtaa kutoa taarifa ya kupotelewa mtoto wao tangu Jumatano ya Desemba 4, mwaka huu.
“Niliwaambia kuwa tumepokea taarifa yao, lakini walisisitiza kwamba twende nyumbani tukatafute, wajumbe wangu walitoka na kwenda nao nyumbani lakini baadaye wakashauri kwenda Kituo cha Polisi Gogoni,” alisema Sabuni.
Aliongeza kuwa walipokwenda polisi na kuwapa taarifa hiyo, waliwaambia kuwa wamepokea taarifa lakini hawawezi kufungua kesi kwa sababu anayetolewa taarifa ni mtu mzima huenda yuko mahali, hivyo warudi waendelee kutafuta.
Alieleza kuwa waliporudi nyumbani kuendelea kutafuta, walipita eneo ambalo lilikuwa na miwa na limelimwa, wakati wakitembea meta 15 kutoka ilipo nyumba waliona eneo limeinuka na walipokanyaga lilikuwa linatitia.
Kutokana na hali hiyo, walichukua mti kwa ajili ya kufukua ndipo waliona mwili ukiwa juu juu ukiwa umeanza kuvimba na kutoa harufu.
“Tuliona mwili saa 9:00 alasiri, si kwamba mwili ulipofunikwa ilifika hata meta mbili, ulifunikwafunikwa tu. Baada ya kuona hivi, tuliwasiliana na jeshi la polisi wakaja na kufukua mwili na kisha waliuchukua na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) kwa uchunguzi zaidi,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Sabuni, mume wa Magdalena alichukuliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu kifo hicho na kwamba mfanyakazi wa ndani wa kiume ambaye walikuwa wakiishi naye, hakuonekana baada ya tukio hilo hivyo anatafutwa.
Kadhalika, mwenyekiti wa mtaa alisema wakati wa ufukuaji wa mwili wa Magdalena, mume wake, alikuwepo na alionesha kushangazwa na tukio hilo.
“Mumewe alituambia kuwa siku ya Jumatano mkewe aliondoka kwenda kazini na baadaye alipokuwa akimpigia simu hakuwa anapokea na wakati mwingine simu yake ilikuwa haipatikani. Alidai alianza kumtafuta kuanzia Jumatano usiku, Alhamisi mchana na usiku,’’ alifafanua Sabuni.
Kwa mujibu wa Sabuni, hawafahamu kama kulikuwa na ugomvi kati ya Magdalena na mumewe na kwamba waliishi katika eneo hilo kwa takribani miaka sita.
“Kwa namna kifo kilivyotokea, kila mtu anazungumza lake, ni bora kuuguza unajua mtu anaumwa lakini kifo hiki kilivyotokea hatujui sababu ni nini, nasi tunasubiri taarifa ya polisi,’’ alisema mwenyekiti wa mtaa.
Hata hivyo, kaka wa Magdalena, Levi alisema suala hilo linahusisha polisi hivyo hawezi kutoa taarifa zinazohusiana na kifo hicho. Aliomba suala hilo liachiwe familia kwa kuwa huyo ni dada yao na wana majonzi.
“Polisi wanafanya kazi yao, watakuja na ripoti zao na kufanya decision (uamuzi) yao, watajua wenyewe, tunaomba hili suala libaki kuwa la familia kama vile ndugu yako. Najua unatafuta habari ni kazi yako, naomba kama binadamu mwenzako tumalizane nalo,’’ alisisitiza.
Aliongeza kuwa kama kuna kesi, polisi watashughulikia na kama ni haki itatendeka.
Katika hatua nyingine, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Temeke, Dk Joseph Kimaro alitangaza kifo cha mtumishi huyo na kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wenzake kwa msiba huo mzito.