Mfuko wa AHMMEF kuboresha tafiti, miundombinu Muhas

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS (AHMMEF) aliouzindua leo utafanikisha ujenzi wa miundombinu ya chuo, tafiti na gharama za hosteli za wanafunzi na masuala mengine.
Akizungumza leo Februari 29, 2025 jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mfuko huo na kongamano la kumuenzi Hayati Dk Mwinyi aliyekuwa mkuu wa chuo wa kwanza na Rais wa awamu ya pili, Dk Mwinyi amesema mfuko huo utasaidia kupunguza utegemezi.
Amesema fedha zitakazopatikana zitasaidia kudhamini wanafunzi, utafiti na uboreshaji wa miundombini chuoni hapo hivyo kuchangia ustawi na maendeleo endelevu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Dk Mwinyi amesema chuo hicho kimekuwa kikitekeleza majukumu yake ya kufundisha, kutafiti na kutoa huduma za afya na kwamba kimekuwa kikizalisha wataalamu mbalimbali wa afya.
“Kimekuwa chuo pekee nchini kinachofundisha wataalamu wa afya kwa ngazi zote na kina programu 20 za kibobezi ikiwemo upasuaji wa moyo, ubongo, figo na nyingine nyingi,” alisisitiza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Adolf Mkenda amesema kuwa matamanio ya serikali ni kuhakikisha eneo la Mloganzila linakuwa mji wa taaluma za afya ifikapo mwaka 2050.
Alisema ujenzi wa Ndaki ya Tiba chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya kujifunzia na hosteli utakaokamilika Juni
Alisema lengo ni kuongeza wataalamu wa afya ndani na nje ya Tanzania wenye uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali za afya kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya tabia nchi.
“Serikali inazidi kupambana na kupanua soko la ajira kuhakikisha wahitimu wetu wanaajiriwa punde wanapomaliza mafunzo yao. Tutakuwa na vituo vya umahiri hivyo kwa kufundisha vizuri, wahitimu wetu wanaweza kuajiriwa hapa au nje ya nchi,” alieleza.
Prof Mkenda amesema wizara yake ipo tayari kuchangia mfuko huo, hivyo kabla ya kwenda kuchangiwa na taasisi zingine ni vyema ukapita kwanza katika wizara yake kuchangiwa.
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema kuwa wamekamilisha usajili wa mfuko huo kwa ajili ya kuanza kupokea fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo, wahitimu na watu binafsi.
“Mfuko huu ni kwa ajili ya kutoa msaada wa kifedha wa kudumu kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma kuhakikisha kuwa MUHAS inaendelea kuwa chuo bora cha elimu ya afya na sayansi shirikishi, utoaji huduma za afya na utafiti nchini Tanzania,” amesema.



