Mfumo wa MIMIS waimarisha ukaguzi magari

DODOMA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyombo vya Moto (MIMIS) yameendelea kuboresha ufanisi wa ukaguzi wa magari na usimamizi wa taarifa katika Jeshi la Polisi.
Ayoub amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa za utekelezaji wa MIMIS wa Jeshi la Polisi na maendeleo ya Chuo cha Idara ya Uhamiaji cha Raphael Kubaga mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU).

Amesema MIMIS umewezesha kurahisisha upatikanaji na utunzaji wa taarifa za vyombo vya moto, kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa na kuimarisha usalama barabarani kupitia matumizi ya teknolojia katika shughuli za ukaguzi wa magari.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, matumizi ya mfumo huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi katika usimamizi na ukaguzi wa vyombo vya moto, huku taarifa za ukaguzi zikihifadhiwa kwa usahihi na kusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Waziri amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha Chuo cha Idara ya Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo mkoani Tanga, kwa lengo la kuimarisha mazingira ya mafunzo na kuongeza uwezo wa chuo hicho kutekeleza majukumu yake.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2025/2026, Serikali imewekeza Sh bilioni 1.2 katika chuo hicho, huku Sh bilioni 2.36 zikitengwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuendeleza chuo hicho.

Katika eneo la mafunzo, amesema jumla ya askari 3,807 wamepata mafunzo ya awali, huku askari na maafisa 1,806 wakipatiwa mafunzo ya uongozi.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ujuzi na uwezo wa kiutendaji wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, amesema chuo hicho kimepanda miti 10,000 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Najma Murtaza Giga, kwa niaba ya Kamati, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha matumizi ya mfumo wa MIMIS ili kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa vyombo vya moto.

Kamati pia imepongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kwa mikakati ya kutumia MIMIS kuboresha ukaguzi wa vyombo vya moto na kuchangia kupunguza ajali za barabarani.
Aidha, Kamati imeipongeza Idara ya Uhamiaji kwa hatua za kuendeleza na kuimarisha Chuo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga.



