Mganda, Mkenya washinda mbio za magari

USHINDI wa mbio za magari za taifa (Asas National Rally Championship) na ule wa Mashindano ya Magari Afrika ( Africa Rally Championship) umewanyong’onyeza watanzania baada ya kwenda kwa madereva wa Uganda na Kenya.

Mbio hizo zilizofanyika kwa siku mbili kwa udhamini wa kampuni ya Asas katika vituo viwili mkoani Iringa, Matembo Asas Farm na Msitu wa Taifa wa Saohill zilifanywa kwa pamoja zikishirikisha madereva 17 ambao kati yao saba walishiriki mbio za Afrika na waliobaki za taifa.

Advertisement

Na kati ya madereva hao, watano walitoka Kenya, Uganda na Ufaransa. Wakati dereva Karan Patel na msoma ramani wake Tauseef Khan kutokz Kenya walitwaa ubingwa wa Afrika, dereva Jas Mangat kutoka Uganda na msoma ramani wake Jules Escatefigue wa Ufaransa walishinda mbio za Taifa.

Mtanzania Ahamed Huwel aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwa mshindi wa mbio za Taifa, aliishia njiani baada ya gari yake aina ya Ford Fiesta Proto kupata hitilafu kubwa na kushindwa kuendelea na mashindano hayo.

Akikabidhi zawadi kwa washindi Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amelitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lihakikishe kuwa linakutana na Chama cha Mbio za Magari chini (AAT) ili kuangalia namna ya kuwsaidia wapate hekari 20 waliizoomba kwa ajili ya eneo la mafunzo na mazoezi.

Amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imepewa jukumu la kusimamia michezo yote nchini ili iwe na ufanisi mkubwa kwa kuwa michezo ni ajira na ina mchango mkubwa katika pato la Taifa.

“Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatutaka kusimamia michezo yote nchini. Na sisi tumejipanga kuhakikisha maono yake katika michezo yote yanatimia,” amsema.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa amesema wilaya ya mufindi ina maeneo mazuri kwa uwekezaji wa mchezo huo wa magari na amewakaribisha AAT wilayani humo.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Saohill, Tebby Yoramu amesema Wakalawa Misitu Tanzania (TFS) inawakaribisha wadau wote kutembelea shamba hilo akisema kuna fursa nyingi za uwekezaji ukiwemo uzalishaji wa malighafi mbalimbali zitokanazo na miti.

“Lakini pia shamba letu lina miundombinu mizuri ya barabara zinazovutia mashindano hayo ya magari ambayo ni muhimu kwa kutangaza uwekezaji na utalii,” amesema.

Amesema shamba hilo lipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza michezo nchini zikiwemo mbio hizo za magari ikitambua kwamba michezo ni ajira na uchumi.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni za Asas, Ahamed Asas amepongeza namna mashindano hayo yalivyofanyika kwa usalama na kuvutia watazamaji wengi kutoka ndani na nje ya mkoa huku akiahidi kampuni zao kuendelea kuyadhamini mwakani.

Asas amewapongeza madereva kutoka nje kwa ushindi wa mashindano hayo akisema utaongeza chachu kwa madereva wa kitanzania kununua magari ya kisasa ili kuwawezesha kushinda siku za usoni.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *