Mgombea anapoahidi kuwashushia wapigakura senene!

SIKU zinahesabika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025. Kampeni zimeshaanza kama inavyooneshwa katika ratiba iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Nimeona ni vyema kuwatakia kila la heri wagombea wote wa udiwani, ubunge na urais katika kam- peni za uchaguzi’.Hii ni fursa yao ya kuwashawishi wananchi kwa kuwaeleza ni namna gani wataleta mabadiliko. Mgombea yeyote aliye na nia ya kuwatumikia wananchi, ahakikishe ahadi ni za kutekelezeka na zenye kuleta maendeleo katika jamii; si vyema kutoa ahadi ambazo hawezi kuzitekeleza.

Licha ya ahadi zisizotekelezwa kuwa kero kwa wapigakura, vilevile zina matokeo hasi kwa mgombea mwenyewe kwa namna tofauti ikiwamo kupoteza imani ya wananchi na kusababisha kukosa kuchaguliwa tena. Wagombea hawana budi kukumbuka kwamba miaka mitano haiko mbali. Wakati huo mtakapoja ribu kuwania nafasi tena, wananchi watakumbuka msimu wenu wa kutoa ahadi bila utekelezaji.

Watambue kwamba zama hizi si kama zile ambazo ilikuwa vigumu kuweka kumbukumbu ya mambo aliyoahidi mgombea. Sasa hivi kila Mtanzania ana ‘daftari la kumbukumbu’ ambalo ni mitandao ya kijamii ambayo yanahifadhi kila sauti na matendo yote yatakayojiri katika kampeni.

Chonde wagombea msitumie mikutano ya kampeni kuwafanya wananchi wachoke na washindwe kuamini siasa na hatimaye kusababisha kushuka kwa kiwango cha uwajibikaji wa viongozi na kudhoofisha demokrasia nchini. Wananchi wanahitaji viongozi wa kweli, wasiojigamba kwa ahadi kubwa na ngumu zisizowezekana. SOMA: Kumekucha kampeni za Uchaguzi Mkuu

Ndugu wagombea, hakikisheni mnawaambia wananchi ukweli na mipango yenu halisi ya kuwahudumia Wananchi wanastahili heshima na uadilifu wenu. Kama nilivyowahi kuhoji katika safu hii, ‘Magoti ya watiania yatakuwa endelevu baada ya Oktoba 29?’ na leo naendelea kuhoji swali hili huku nikiendelea kuwahadharisha wagombea dhidi ya ‘usanii’ katika kampeni.

Nilihoji wakati wa kipindi cha watiania kuomba kura kwa wajumbe ambacho baadhi walilazimika kupiga magoti katika harakati za kubembeleza kura ya ‘ndiyo’.Hata wasio na utamaduni huo walilazimika kufanya hivyo! Hoja yangu ilikuwa ni kuwahadharisha dhidi ya kufanya maigizo nikisisitiza kwamba matendo hayo yawe endelevu hata baada ya kupata ubunge, uwakilishi na udiwani.

Kwamba baada ya kupata hizo nafasi, warudi kwenye kata na majimbo wawashukuru wapigakura wakiendelea kuwapigia magoti kwa kuwaomba wawatume mambo wa- nayotaka yafikishwe bungeni. Isije ikatokea baada ya kupata kura za ndiyo, wananchi ndio wabaki kuwapigia magoti na kuwaita ‘wa- heshimiwa’ bila kufanyiwa maende- leo yoyote kama ilivyokuwa wakati wa kuomba kura.

Kwa hiyo hata sasa, naendelea kuwasisitiza wagombea waliopitishwa kwamba wananchi hawahitaji maigizo. Nawahadharisha nikitaka watambue kwamba katika zama hizi, wananchi wana uelewa wa kutosha. Hizi si zama zile ambazo niliwahi kusikia simulizi kuhusu mgombea mmoja wa ubunge katika jimbo fulani (enzi za chama kimoja) aliwaahidi wagombea kuwa wakimchagua atawashushia senene.

Aliangalia kitu ambacho wananchi wa jimbo lake wanapenda na kukithamini, akaona senene ni chaku- la muhimu kwa wananchi wa jimbo hilo. Kwa kuwa wadudu (chakula) hao hupatikana kwa msimu, akaona katika kutafuta kugusa mioyo ya wa- nanchi, basi awaambie wakimchagua senene watapatikana wakati wote! Hizi ndizo ahadi ngumu; ahadi za kujibebesha mzigo mkubwa.

Ahadi zisizo hata kwenye ilani ya vyama vyao. Ahadi za kutenda miujiza ambayo mwanadamu yeyote hawezi, isipokuwa Mungu. Chonde wagombea, kampeni zinakaribia msije kutuahidi wapigakura kwamba mtatuongezea vimo vya urefu wetu au kuhamisha milima na mabonde yanayotuzunguka kwa mikono yenu au kuahidi kutushushia wapigakura senene.

Ahidini mambo yaliyo ndani ya uwezo wenu na hasa yanayoakisi ilani za vyama vyenu. Vivyo hivyo vyama vya siasa, ilani zake zizungumze mambo yenye uhalisia kwa maana yanayotekelezeka na si kunogesha kampeni kwa ahadi zinazochekesha kama si kushangaza

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button