Aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa zahanati hatiani kwa kughushi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara katika shauri la uhujumu uchumi Na. 15921/2025) imemtia hatiani mshtakiwa, MOHAMED TWALIB BAYA kwa kosa la kughushi k/f cha 333,335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2022
Mshitakiwa alighushi sahihi za watia saini katika akaunti ya Zahanati ya Endwagwa na kuchukua sh 8,015,000/= ambazo alizifanyia ubadhirifu.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Babati, Victor Kimario amemtia hatiani mshtakiwa baada ya mshtakiwa huyo kufanya makubaliano (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hapo awali alishtakiwa kwa kufanya ubadhirifu sh 8,015,000/= kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyorejewa mwaka 2022 pamoja na kuisababishia Mamlaka hasara kinyume na Aya 10(1) katika jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200 Marejeo ya 2022].
Pia alishtakiwa kwa makosa ya kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya sheria ya kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2022.
Mshtakiwa amepewa adhabu ya kulipa faini sh laki mbili (200,000) au akishindwa atumikie kifungo cha gerezani kwa muda wa mwaka mmoja pamoja kurejesha fedha alizozifanyia ubadhilifu sh 8,0150,000/= kwa muathirika.
Hadi hukumu inasomwa mshtakiwa amerejesha sh 4,000,000/= katika akaunti ya Zahanati ya Endangwe (Muathirika) iliyopo Bank ya NMB na kiasi kilichobaki atakirejesha kabla au ndani ya mwezi mmoja.
Shauri hilo lilikuwa linaendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Manyara ambao ni Neema Gembe, Davis Masambu na Catherine Ngessy.



