Miaka mitano ya fursa mpya uchumi wa Tanzania

DAR ES SALAAM; Rudisha  fikra nyuma kwa Tanzania ya mwaka 2021 yenye vijana waliokuwa wanajiuliza maswali kuhusu suala la ajira ziko wapi?

Maswali yalikuwa mengi zaidi ya majibu. wasiwasi ulikuwa mwingi kuliko uhakika. Vichwa vingi vilijiuliza:  Tutavuka salama kweli kutatua tatizo la ajira? Huku wengine wakienda mbali na kuliita bomu. Ungana nami SYLIVESTRE DOMASA katika makala haya hatua kwa hatua kuhusu miaka mitano ya fursa mpya uchumi wa Tanzania.

Vijana na fursa za ajira

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya vijana walikuwa wakimaliza shule, vyuo vya kati na vyuo vikuu huku wakikabiliwa na soko la ajira lenye ushindani mkubwa.

Kwa wengi, mafanikio yalitafsiriwa kwa kupata ajira serikalini au katika kampuni binafsi. Kwa wengine, biashara ndogo ndogo zisizo rasmi zilikuwa njia pekee ya kujikimu.

Miaka mitano baadaye, changamoto ya ajira bado ipo, lakini jambo lililobadilika ni namna taifa linavyoitazama.

Leo mjadala kuhusu vijana hauhusu tena ajira pekee. Unahusu fursa. Unahusu mitaji. Unahusu ujuzi. Unahusu teknolojia. Unahusu uwekezaji. Unahusu ubunifu. Na kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, unahusu taasisi maalumu ya Serikali yenye jukumu la kusimamia maendeleo ya vijana.

Kuanzishwa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana mwaka 2025 ni moja ya hatua kubwa zaidi za kisera zilizochukuliwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Ni ishara kwamba ajenda ya vijana imehama kutoka kuwa sehemu ya sera za wizara mbalimbali na kuwa agenda ya taifa inayojitegemea.

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo Tanzania ina vijana zaidi ya milioni 20.6 wenye umri wa miaka 15 hadi 35, sawa na asilimia 34.4 ya wananchi wote.

Zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya taifa inatokana na kundi hili. Kwa lugha nyingine, mustakabali wa uchumi wa Tanzania unategemea kwa kiwango kikubwa namna vijana watakavyoshiriki katika uzalishaji, ubunifu na uwekezaji.

Lakini safari hii haikuanza mwaka 2026.

Kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya miaka mitano ya uwekezaji katika miundombinu, mageuzi ya sera, ukuaji wa sekta binafsi na programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi.

Kutoka kujenga uchumi hadi kujenga fursa

Katika miaka ya mwanzo ya Serikali ya Awamu ya Sita, kipaumbele kikubwa kilikuwa kufufua uchumi, kuvutia uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa madaraja, barabara, viwanja vya ndege, miradi ya maji na uwekezaji katika sekta za madini, nishati na viwanda viliendelea kupewa kipaumbele katika bajeti za taifa.

Kwa mtazamo wa kawaida, miradi hiyo inaweza kuonekana kama uwekezaji wa miundombinu. Lakini kwa vijana, miradi hiyo imekuwa chanzo cha ajira, mafunzo ya vitendo na biashara.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri.

Katika maeneo mengi, vijana wamepata nafasi za kazi kama mafundi, wahandisi, wachomeleaji, madereva, mafundi umeme, wahudumu wa huduma mbalimbali na wasambazaji wa bidhaa kwenye maeneo ya miradi.

Wakati huo huo, uwekezaji umeendelea kuongezeka nchini.

Takwimu za Tanzania Investment Centre (TIC) na baadaye TISEZA zinaonesha ongezeko la miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa katika kipindi cha miaka ya karibuni, hali iliyochangia kuongezeka kwa ajira zinazotokana na sekta binafsi.

Hii imekuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kupanua nafasi za kazi nje ya ajira za moja kwa moja za serikali.

Umeme na Uchumi wa Vijana

Miongoni mwa mabadiliko makubwa yaliyotokea katika miaka mitano iliyopita ni upanuzi wa upatikanaji wa umeme.

Uwezo wa uzalishaji umeme umeongezeka kutoka megawati 1,601 mwaka 2021 hadi zaidi ya megawati 4,500 mwaka 2026. Vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimefikiwa na umeme huku mamilioni ya wananchi wakiongezwa kwenye mtandao wa TANESCO.

Athari za uwekezaji huo zinaonekana moja kwa moja katika maisha ya vijana.

Katika Kitongoji cha Kisendema wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, mwakilishi wa vijana Athumani Sadik anasema ujio wa umeme umefungua fursa mpya ambazo zamani hazikuwepo.

 

Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria kuzima majenereta na kuzindua umeme wa Gridi ya Taifa kwa Mkoa wa Kigoma kwenye hafla iliyofanyika Kasulu Mjini.

 

“Umeme umetupa fursa za uchomeaji, useremala, biashara za baridi na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa vigumu kuanzisha.”

Kauli hiyo inaonyesha jinsi uwekezaji wa miundombinu unavyoweza kubadilika na kuwa ajira na kipato kwa vijana walioko mbali na miji mikubwa.

Kutoka Watafuta Kazi Hadi Waajiri

Labda mabadiliko makubwa zaidi katika kipindi hiki ni kuanza kubadilika kwa mtazamo kuhusu ajira.

Kwa muda mrefu, mafanikio ya kijana yalipimwa kwa uwezo wake wa kupata kazi.

Leo, Serikali inazungumzia zaidi uwezo wa vijana kuanzisha biashara, kuwekeza na kuajiri wengine.

Mwaka 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza mpango wa uwezeshaji wa vijana wenye thamani ya Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kusaidia biashara ndogo, za kati na kampuni changa zinazoanzishwa na vijana.

Kupitia mpango huo, Serikali inalenga kuondoa baadhi ya vikwazo vikubwa vinavyowakabili vijana, hususan ukosefu wa mitaji.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, hadi Aprili 2026 zaidi ya maombi 30,384 ya mikopo ya miradi ya vijana yalikuwa yamepokelewa. Katika awamu ya kwanza, Shilingi bilioni 48.6 zilitolewa kwa miradi mbalimbali ya vijana katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, viwanda, TEHAMA na ubunifu.

Aidha, vikundi 5,199 vya vijana vilinufaika na zaidi ya Shilingi bilioni 52.1 kupitia mikopo ya asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Takwimu hizi zinaonesha juhudi za kujenga mfumo ambao unawawezesha vijana kuwa wazalishaji wa utajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

Kilimo Kinabadilisha Taswira

Kwa muda mrefu, vijana wengi walikiona kilimo kama sekta isiyo na mvuto.

Lakini miaka ya karibuni imeanza kubadilisha mtazamo huo.

Kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), Serikali imeanza kuwapa vijana ardhi, mafunzo, teknolojia na fursa za kuingia katika kilimo biashara.

Mabadiliko hayo yalikuwa yanaandaliwa hata kabla ya programu hiyo kuanzishwa.

Mwaka 2022, Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, alieleza namna benki hiyo ilivyokuwa ikijipanga kuwasaidia vijana kuingia katika kilimo biashara.

“Vijana wenye sifa za kukopesheka watawezeshwa kuanzia maandalizi ya mashamba, pembejeo, masoko na hata uchakataji wa mazao. Tunatoa mikopo kwenye mnyororo mzima wa kilimo kuanzia kulima hadi kutafuta masoko ya mazao.”

Aliyekuwa Makamu wa Dk Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dk Samia Suluhu Hassan Mlazo/ Ndogowe uliyopo Kijiji cha Mlazo Wilaya ya Chamwino akiwa ziarani mkoani Dodoma.

Kauli hiyo inaonyesha mabadiliko ya namna taasisi za fedha zinavyotazama vijana; si kama wakopaji wa kawaida, bali kama wawekezaji wa baadaye.

Kwa vijana wengi waliokuwa wakikimbilia mijini kutafuta ajira, kilimo sasa kinaanza kuonekana kama eneo la biashara na uwekezaji.

Uchumi wa Kidijitali na Ajira Mpya

Kama kuna eneo ambalo limebadilika kwa kasi kubwa zaidi katika miaka mitano iliyopita, basi ni uchumi wa kidijitali.

Leo, maelfu ya vijana wanapata kipato kupitia utengenezaji wa maudhui mtandaoni, usimamizi wa mitandao ya kijamii, biashara za mtandaoni, usanifu wa picha, utengenezaji wa video, programu za kompyuta na huduma nyingine za kidijitali.

Kutambua mabadiliko hayo, Serikali ilianza kutoa mafunzo maalumu kwa watengeneza maudhui mtandaoni mwaka 2025.

Hatua hiyo ilionesha kuwa uchumi wa ubunifu na teknolojia umeanza kutambuliwa rasmi kama sehemu ya uchumi wa taifa.

Katika mafunzo hayo, vijana walihimizwa kuona teknolojia si kama eneo la burudani pekee bali kama chanzo cha biashara, ajira na uwekezaji.

Kwa mara ya kwanza, kizazi cha vijana kinaweza kufanya kazi kwa wateja walioko nje ya Tanzania bila kuondoka nchini.

Wanawake Vijana Katika Uchumi Mpya

Mabadiliko haya hayawahusu wanaume pekee.

Wanawake vijana nao wanaendelea kutumia fursa zinazotokana na elimu, biashara, teknolojia na ubunifu.

Nancy Sumari, mmoja wa vinara wa uwezeshaji wa vijana nchini, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana uwezo wa kutatua changamoto na kuunda fursa badala ya kusubiri kupewa nafasi.

Kwa upande mwingine, Dkt. Victoria Kisyombe, mwanzilishi wa SELFINA, ameonesha kwa vitendo jinsi upatikanaji wa mitaji na mali za uzalishaji unavyoweza kuwabadilisha wanawake kutoka wafanyakazi wa kawaida hadi wamiliki wa biashara.

Mifano hiyo inaonyesha kuwa ajenda ya vijana na ajenda ya ushiriki wa wanawake katika uchumi haviwezi kutenganishwa.

Vijana Wanasemaje?

Katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka 2025, vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walitoa maoni yao kuhusu mustakabali wa ajira.

Wengi walikiri kuwa fursa zimeongezeka katika sekta za teknolojia, kilimo biashara, biashara na ubunifu.

 

 

Hata hivyo walisisitiza kuwa changamoto bado zipo katika upatikanaji wa taarifa za fursa, mitaji, masoko na mafunzo ya ujuzi.

Hoja hizo zinaonesha kuwa changamoto ya vijana wa Tanzania leo si ukosefu wa ndoto wala ukosefu wa nguvu kazi.

Changamoto kubwa ni namna ya kuunganisha nguvu kazi hiyo na fursa zinazozalishwa na uchumi.

Safari Bado Inaendelea

Serikali inakiri kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana bado kinafikia asilimia 12.2.

Hii ina maana kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Lakini tofauti na miaka mitano iliyopita, Tanzania sasa ina mazingira mapya.

Ina uwekezaji mkubwa wa miundombinu.

Ina programu za uwezeshaji wa vijana.

Ina mifumo ya mikopo.

Ina uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Ina kilimo biashara kinachovutia kizazi kipya.

Na kwa mara ya kwanza, ina taasisi maalumu inayosimamia maendeleo ya vijana.

Miaka mitano iliyopita, mjadala wa vijana ulijikita zaidi katika ukosefu wa ajira.

Leo, mjadala huo unaanza kuhamia katika namna ya kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji, kilimo biashara, TEHAMA, ubunifu, viwanda na uchumi wa kidijitali.

Hiyo ndiyo tofauti kati ya taifa linalozungumzia tatizo la ajira na taifa linalojenga mazingira ya kutengeneza ajira.

Na huenda mafanikio makubwa zaidi ya kipindi cha miaka mitano iliyopita si idadi ya mikopo iliyotolewa wala mafunzo yaliyofanyika, bali ni mabadiliko ya fikra kwamba maendeleo ya Tanzania hayawezi kutenganishwa na maendeleo ya vijana wake.

Kwa taifa ambalo zaidi ya nusu ya nguvu kazi yake ni vijana, huo unaweza kuwa msingi wa safari ya kuelekea uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kuzalisha fursa kwa kizazi kijacho.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button