Michuano ya Gofu kurindima Dar es Salaam Julai 5

MICHUANO ya wazi ya gofu ya “Vodacom Lugalo Open 2024” inatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Julai katika Klabu ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam Leo Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo amesema mashindano hayo yatakuwa ya mfano ambapo klabu zote za mchezo huo nchini na nchi jirani zitashiriki.

Amesema mpaka sasa idadi kubwa ya washiriki wameanza kujiandikisha wakionyesha nia ya ushiriki na anaamini kila klabu itaonyesha upinzani mkubwa.

“Lengo ni kuwafanya wachezaji waweze kuonyesha viwango vyao kupitia shindano hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kufahamiana na watu mbalimbali,”amesema.

Amewashukuru wadhamini wa mashindano hayo na kuwataka watanzania kwenda kwa wingi kujionea vipaji vya washiriki hao, ambapo kutakuwa na makundi ya watoto, wanawake na wakongwe.

Mkuu wa Masoko wa Vodacom Aileen Meena amesema wataendelea kushirikiana na klabu hiyo kuhakikisha wanaufikisha mbali mchezo wa gofu.

Rais wa Chama cha gofu Tanzania (TGU) Gilman Kasiga amesema shindano hilo litasaidia wachezaji watakaofanya vizuri kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

Ameongeza kuwa mchezo wa gofu kwa sasa umeshika kasi tofauti na miaka iliyopita kwa idadi kubwa ya watanzania kujiunga.

Habari Zifananazo

Back to top button