Mifugo kufugwa, kulishwa kisasa

WAUZAJI na wazalishaji wa vyakula vya mifugo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, wamepewa mafunzo ili kuwawezesha kulisha na kufuga kisasa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), iliyopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Stella Bitanyi amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam.

Dk Bitanyi amesema utoaji mafunzo hayo umetokana na malalamiko ambayo Serikali imekuwa ikiyapokea hasa kutoka kwa wafugaji wa kuku ambao wamekuwa wakilalamikia udumavu wa kuku unaohusishwa na ubora hafifu wa vyakula vya mifugo vilivyopo sokoni.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kukagua utekelezaji wa yale waliyoelekezana kwenye mafunzo hayo.

Amesema ufuatiliaji huo utafanywa na kikosi kazi kutoka kwenye wakala huo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara yake ya Nyanda za malisho na vyakula vya Mifugo na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka kwenye Mikoa na Wilaya zote nchini.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Rogers Shengoto amesema Wizara yake imetumia mafunzo hayo kuwasisitiza wadau wote waliopo kwenye tasnia ya vyakula vya Mifugo kuhakikisha wanasajili shughuli zao kwa mujibu wa sheria ya Maeneo ya Malisho sura namba 180 pamoja na kanuni zake.

“Lakini pia msitumie nafaka au rasilimali za vyakula zisizofaa kwa matumizi ya binadamu kutengenezea vyakula vya Mifugo kwa sababu mnyama akiathirika humuathiri pia mlaji anayekula nyama ile,’ amesema.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mzalishaji wa vyakula vya Mifugo, Mohammed Mshana ameishukuru serikali kwa kuwawezesha mafunzo hayo ambapo ameshauri zoezi hilo liwe endelevu ili waweze kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa tija.

Naye mfugaji kutoka Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam, Albina John amesema mafunzo hayo yamemwezesha matumizi sahihi ya chanjo za mifugo.

Hivyo anatarajia kuanza kutibu mifugo yake kwa wakati, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo chanjo alizokuwa akinunua kutoka nje ya nchi zilikuwa hazimfikii kwa wakati.

Mafunzo hayo yamefanyika wiki chache tangu kufanyika kwa operesheni maalum ya ukaguzi wa viwanda na maduka yanayouza vyakula vya Mifugo iliyoendeshwa na wakala huo na kubaini dosari mbalimbali kwa wadau hao wa ufugaji nchini.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button