Mifumo kidijitali kuboresha huduma za sheria

DODOMA: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha utendaji wa taasisi zake na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 22, 2026, jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edwin Enosy Swalle, baada ya kupokea taarifa za utekelezaji wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Swalle amesema matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi hizo yamechangia kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma, uwazi na uwajibikaji.

Amesema kuboreshwa kwa Mfumo wa Usimamizi wa Mafunzo kwa Vitendo (LST-e-FIELD MIS 2026) na mtaala wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ni hatua inayosaidia kuboresha uwezo wa wanafunzi na kutathmini kwa usahihi maarifa wanayopata wakati wa mafunzo.

Aidha, kamati hiyo imeitaka RITA kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa e-RITA, hususan katika usajili na marekebisho ya vyeti vya kuzaliwa pamoja na usajili wa ndoa.

Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Hamis Ulega, akiwasilisha taarifa za taasisi hizo, amesema wizara na taasisi zake zinaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuboresha huduma, kuongeza uwazi na uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Amesema hatua hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayotambua mapinduzi ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya kujenga uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi.

“Wizara na taasisi zake zinaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA. Hili linajidhihirisha kupitia mifumo ya kimkakati inayotumiwa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo katika kusimamia mafunzo ya vitendo,” amesema Ulega.

Katika taarifa yake, Ulega ameeleza hatua zilizochukuliwa kuboresha mfumo wa LST-e-FIELD MIS 2026, matumizi yake na matokeo yaliyopatikana katika kuboresha mafunzo ya vitendo na kuwaandaa wanafunzi kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Pia, amewasilisha taarifa ya RITA kuhusu maboresho ya huduma za usajili na uhifadhi wa kumbukumbu za matukio ya kijamii kupitia mfumo wa e-RITA, unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuimarisha usalama na uaminifu wa taarifa na kudhibiti matumizi ya nyaraka zisizo halali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button