Mikakati kudhibiti udanganyifu huduma za bima izae matunda

SERIKALI imeeleza mkakati wa kukabili udangayifu katika huduma za bima miongoni mwake ikiwa ni mpango wa kuanzisha mahakama au kitengo cha kushughulikia kesi hizo.

Taarifa hiyo ilitolewa wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Umoja wa Wataalamu wa masuala ya Bima (IASIU) jijini Arusha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema hayo alipomwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi kwenye mkutano huo.

Mpango huo wa kuwepo mahakama au kitengo maalumu cha kushughulikia kesi za udanganyifu ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta hii.

Imeelezwa kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), serikali imeanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwemo IASIU tawi la Tanzania kukabili udanganyifu huo.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ya ufuatiliaji na uthibitishaji wa madai ya bima ikiwa ni pamoja na kuanzisha kanzidata ya pamoja.

Ni kwamba zitawekwa kanuni kali dhidi ya kampuni au watu binafsi wanaojihusisha na udanganyifu, kuanzisha mahakama au kitengo cha kushughulikia kesi za udanganyifu wa bima kwa haraka na kwa weledi na kuelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika matumizi ya huduma za bima.

Bima ni sehemu muhimu ya mfumo wa kifedha unaosaidia wananchi kukabiliana na majanga na matatizo ya kifedha yanayoweza kujitokeza. Lakini udanganyifu unaweza kuathiri soko na kuleta hasara kubwa kwa kampuni za bima na wateja halali.

Ndiyo maana tunaona ni sahihi na muhimu kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kudhibiti na kupambana na udanganyifu ili kuhakikisha ufanisi wa huduma na kuimarisha imani ya umma katika sekta ya bima.

Si siri, mazingira ya huduma za bima nchini yanakumbwa na changamoto za udanganyifu, ikiwa ni pamoja na wateja kujifanya kuumia au kupoteza mali kwa nia ya kupata malipo bila msingi halali, au kampuni za bima kujihusisha na vitendo vya kujipatia faida kwa njia zisizo halali.

Udanganyifu huu si tu unaongeza gharama za kuendesha sekta ya bima bali pia unaathiri upatikanaji wa huduma kwa wateja wa hali ya chini na kuharibu sifa ya sekta kwa ujumla.

Hali hii inahitaji hatua madhubuti za kitaasisi na kisheria, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mahakama inayoshughulikia kesi za udanganyifu kama ilivyoelezwa ili kuleta utaratibu wa haraka, wa haki, na wa kuaminika.

Udhibiti madhubuti ukiwapo, utaongeza ufanisi wa mchakato wa malipo, kwani kesi za udanganyifu zitashughulikiwa kwa haraka na kwa uwazi, hivyo kupunguza rufaa na ucheleweshaji usio wa lazima.

Ni matumaini yetu kwamba mikakati hii ya kudhibiti udanganyifu katika bima itazaa matunda na itaimarisha mazingira ya biashara katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button