MAWAZIRI wa Michezo wa Tanzania, Kenya na Uganda wamekutana na timu ya wataalamu kutoka nchi hizo kuweka mikakati ya pamoja kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Kikao hicho kilichofanyika Mjini Mombasa, Kenya leo, Novemba 7, 2023 kinakuwa kikao cha kwanza tangu Tanzania, Kenya na Uganda ziliposhinda ombi la kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.
Kwa upande wa Tanzania kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia.
Wengine ni, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Ally Mayai na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Neema Msitha.
Kenya imewakilishwa na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na Katibu Mkuu, Mhandisi Peter Tum huku Uganda ikiwakilishwa na Rodgers Byamukama ambaye ni Mjumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo.