Mikakati yasukwa sekta za umma, binafsi

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru amesema Serikali inafanya majadiliano ya kimkakati na Benki ya Dunia namna ya kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi yaani PPP.

Mafuru alieleza hayo jijini Dodoma baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkazi, Nathan Belete ambapo walijadili namna bora ya utekelezaji wa sheria ya PPP pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.

Alisema majadiliano hayo ni utekelezaji wa msisitizo na maelekezo yanayotolewa na Rais Samia Suluhu kuwa sasa ni wakati wa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.

“Serikali imeanza majadiliano ya awamu ya pili na Benki ya Dunia kuhusu msaada ambao umejielekeza kwenye sekta za miundombinu na sekta zitakazoboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.” alisema Mafuru.

Aidha, alibainisha kuwa Sheria ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) inafanyiwa marekebisho ili iweze kuwa shindani, ambayo itaweza kuvutia mitaji ya Sekta Binafsi na hatimaye kiwezesha sekta hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete alisema benki hiyo imeamua kujadiliana na Tanzania kuhusu namna bora ya utekelezaji wa miradi kwa njia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x