Mikoa sita inayoongoza kwa bangi yatajwa

SERIKALI imetaja mikoa sita inayoongoza kulima bangi na imetangaza vita dhidi ya wanaofanya biashara hiyo haramu baada ya utafiti kubaini ndio dawa ya kulevya inayoongoza kulimwa na kutumika zaidi nchini.

Mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Iringa, Morogoro na Manyara inayolima bangi kibiashara kwa ajili ya kuuza nje na Mara na Ruvuma inayolima na kuuza ndani ya nchi.

Aidha, serikali imegundua kuna watu wanatumia bangi kutengeneza bidhaa za chakula kama sharbati, keki, biskuti, asali na majani ya chai na tayari hatua za kisheria zimechukuliwa kwa watu watatu na mapambano yanaendelea.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari bungeni, Dodoma baada ya kuwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2022.

Taarifa hiyo iliandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Jenista akizungumza kuhusu taarifa hiyo, alisema serikali imegundua kupitia utafiti kuwa bangi ndio dawa ya kulevya inayoongoza kutumika zaidi nchini na inaathiri kundi kubwa la vijana.

Alisema mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara inalima bangi kama zao la biashara kwa ajili ya kuuza nje na wanakaa na taasisi nyingine ikiwemo Wizara ya Kilimo kuona namna ya kuwawezesha kulima mazao mbadala.

Alisema mkoa wa Mara na Ruvuma wanalima kwa matumizi ya ndani.

Jenista alisema kwa kutambua unyeti wa tatizo hilo, serikali imefanikiwa kuandaa mwongozo maalumu wa utoaji elimu na tiba kwa waraibu ambapo mwaka 2022 zaidi ya 871 walipata tiba na 245 kati yao waliunganishwa na vyuo vya ufundi ili wajiajiri.

Alisema pia serikali imetenga Sh bilioni 8.7 kwa ajili ya kujenga vituo vya urekebu kubadili tabia za uraibu za vijana na kujenga pia vituo vya mafunzo ya ufundi ili kuwasaidia watakaopona kufanya shughuli za kiuchumi kujiingizia kipato.

Kwa kuanzia, Jenista alisema vituo vitajengwa katika mikoa mitano ya awamu ya kwanza ambayo ni Shinyanga, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha kwa gharama ya Sh bilioni sita na Sh bilioni 2.7 zitajenga kituo cha urekebu na ufundi jijini Dodoma.

Kuhusu bangi kutengenezea vyakula, Jenista alisema operesheni maalumu zitaendelea ikiwemo za kiutafiti na ukamataji katika maeneo yanayoongoza kwa matumizi na kilimo cha bangi.

“Tayari kuna hatua zimechukuliwa na kuna raia wa kigeni na mke wake Mtanzania walikamatwa Arusha wakitengeneza keki, biskuti na asali zimepakiwa kwenda nje ya nchi na wamefungwa miaka 30 jela.

“Ninachotaka kusema kwa wananchi ni kwamba serikali yao ipo makini na imetangaza vita dhidi ya wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, niwaombe wasamaria wema waendelee kutoa taarifa kwa serikali wanapobaini watu hawa,” alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mwaka 2022 serikali imeteketeza ekari 179 za mashamba ya bangi na tani 20.58 za dawa hizo zilikamatwa.

Aidha, Jenista alisema operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, zilifanikisha kukamata tani 15.2 za mirungi, kilo 254.7 za heroin na kilo 1.7 ya cocaine.

Alisema wamekamata dawa ya kulevya aina mpya ya methamphetamine ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2021 zilikamatwa kilo 430.8 na kufuatiwa na gramu 968.7 ambazo zilikamatwa mwaka 2022. Pia mwaka 2022 dawa nyingine ngeni nchini inayojulikana kama mescaline ilikamatwa kilogramu 56.

Habari Zifananazo

Back to top button