BAADHI ya viongozi wa serikali za mitaa Kata ya Bulega Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamesema tatizo la mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) imekuwa chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika.
Kero hiyo imewasilishwa na viongozi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji na kata ya Bulega wilayani humo maalum ili kutoa elimu katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (MSLAC).
Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Bulega, Andrea Anthony amesema suala la mikopo umiza hii limevuruga ndoa nyingi na wao kama viongozi wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutoka kwa wanandoa kujihusisha na mikopo umiza.
Andrea amesema baadhi ya kina mama au kina baba wa familia wanakwenda kukopa na kuweka dhamana mali za familia bila kumshirikisha mwenza ambapo matokeo yake yamekuwa ni taharuki mkopo usiporejeshwa.
“Kwenye maeneo yetu haya wanaweka mpaka vitanda, nyumba, Tv, viti, makochi, sasa anaposhindwa kurejesha zile fedha, tayari wanakuja wale wakopeshaji kwa ajili ya kuja kubeba vile vitu ambavyo aliviweka dhamana.
“Sasa wanapokuja kuchukua hivi vitu muhimu, kwa sababu alikopa bila kushirikisha mme anakuwa na hofu kwamba hizi mali zikija kuchukuliwa itakuwaje, matokeo yake mama analazimika kukimbia familia.
“Mwanaume anaporudi nyumbani anashangaa tu anakuta mama hayupo amekwenda wapi haelewi, kumbe amekimbia deni ambalo mama alikopa bila kumwambia, na ndio mwanzo wa ndoa kuvurugika”, amesema Andrea.
Amekiri kuwa mpaka sasa kwenye eneo lake zipo ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya mikopo umiza ambapo wakopeshwaji wanalazimishwa na taasisi za mikopo kuanza kurejesha ndani ya siku chache kwa riba kubwa.
Diwani wa kata ya Bulega, Eric Kagoma amesema suala la mikopo umiza linachagizwa na michezo ya vikoba ambapo wahusika hulazimika kuchukua fedha pasipo kumshiriisha mwenza wa familia kisha kuweka dhamani mali za ndani.
“Kwa elimu hii ya msaada wa kisheria ya mama samia nafarijika kwa sababu kina mama na kina baba wamefikiwa na hivo elimu hii itasaidia kupunguza migogoro ya familia,”.
Wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Esther Safari amesema kwa mali ambazo zinamilikiwa na familia ama zina maslahi kwa wanandoa, endapo mwanandoa mmoja atachukua mkopo anapaswa kutoa taarifa kwa mwenza.
“Kama mali ambayo anaiweka dhamana lazima kuwe na taarifa kwa wanandoa, ndio maana tunashauri hata kwenye mauziano ya aridhi, ili yale mauziano yawe rasmi lazima mwanadoa naye atoe ridhaa yake.
“Hii inasaidia kwamba hata kama kuna shida inatokea kwa huyu mwenza basi atambue kwamba siyo kitu kigeni lakini pia tunawashauri watu wakope kwa sababu maalum” amesema Esther.
Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) Majid Kangile amewatahadharisha wananchi juu ya taasisi zinazotoa mikopo kwani nyingi hazifuati taratibu na sheria za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nitoe rai kwa taasisi zinazotoa mikopo, toeni mikopo hii kwa mjibu wa sheria zilizowekwa, siyo wewe unaamua kutoa mikopo na unafanya wewe unavyotaka kwa sababu upo ndani ndani (vijijini) serikali ina mkono mrefu”, amesema.
MWISHO