Milango yafunguliwa mikopo wachimbaji Geita

OFISI ya Waziri Mkuu imewahimiza wachimbaji wadogo wa madini kuchangamkia fursa ya mkopo unaotolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuanzisha au kuimarisha miradi ya uzalishaji mali kwa njia salama na endelevu.
Mkopo huo unatolewa mahsusi kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa tija, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita za kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa Vijana.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Daudi Silasi amesema hayo wakati wa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi wachimbaji wadogo mkoani Geita.

“Tunawahimiza wachimbaji wadogo, hasa vijana, kujiunga katika vikundi, kuandaa maandiko ya miradi na kuwasilisha ofisini, mkikidhi vigezo mtapewa fedha kulingana na ukubwa wa mradi”, amesema na kuongeza;
“Lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huo ni kuwawezesha vijana kiuchumi kwa njia ya kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu”.
Akizungumzia mikopo hiyo, mchimbaji mdogo wa madini Hellen Josephat ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu na fursa za mikopo zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Naye, Alphonce Daniel amekiri mafunzo na elimu kuhusu fursa za mikopo na ujasiriamali kwa wachimbaji wadogo imewapa uelewa wa kuandaa maandiko ya miradi na kufuata taratibu sahihi za kisheria ili kupata mkopo.



