DAR ES SALAAM :Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2024, miradi 354 kati ya miradi 998 ya maji iliyopokea fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji imekamilishwa na hivyo kuwanufaisha wananchi takribani milioni 5.3 kwa huduma bora za maji.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji, Wakili Haji Nandule ameyabainisha hayo wakati wa kikao cha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kilichofanyika leo jijini Dar es salaam kilichoandaliwa na ofisi ya msajili wa hazina na kuongeza kuwa mfuko umeendelea kutekeleza miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji ambapo takribani miradi 104 ya uhifadhi na uendelezaji wa vyanzo vya maji imetekelezwa.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Maji, Prosper Buchafwe amesisitiza kuwa kwa kutambua umuhimu wa huduma za maji serikali itaendelea kusimamia miundombinu ya maji ili kuzuia upotevu pamoja na wizi wa maji ili kuwezesha huduma hizo kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri (TEF) Deudatus Balile amesema mkutano huo umewapa mwanga wahariri wa vyombo vya habari kuuelewa vizuri mfuko huo hivyo vyombo vya habari vitaendelea kusisitiza juu ya namna mfuko unavyofanya kazi na kuweza kuwaondolea wananchi kero ya maji katika baadhi ya maeneo hapa nchini.