Miradi ya Sh bilioni 4 yahitaji maboresho Kagera

TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefuatilia miradi 19 yenye zaidi ya Sh bilioni 6.1 kwa kipindi cha mwezi Oktoba – Desemba 2023.

Kati ya hiyo miradi 16 yenye zaidi ya Sh bilioni 4.2 imebainika kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho.

Kamanda wa Takukuru mkoani Kagera, Pilly Mwakasege amesema miradi iliyofuatiliwa ni ya maji, ujenzi wa shule mpya za sekondari na msingi, zahanati na vituo vya afya ambapo miradi yenye upungufu inahitaji marekebisho ya haraka.

Advertisement

Alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.50 ya fedha za miradi ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 18.77 ya miradi hiyo, ukilinganisha na kipindi cha Julai – Septemba mwaka 2022/2023.

Alisema kwa kipindi hicho walipokea malalamiko 92 kati ya hayo 58 hayahusiani na  rushwa ambapo 34 yanahusu rushwa na majalada yamefunguliwa huku majalada  20 uchunguzi wake umekamilika na hatua stahiki zinatarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Idara zilizolalamikiwa ni halmashauri ambapo idara ya fedha kesi moja, elimu 10, afya saba, utawala 12,biashara moja, kilimo nane, ardhi saba, mazingira tatu na mengine yalihusu sekta binafsi ambayo ni 12, maji tatu, ujenzi tisa, maliasili saba, nishati moja, uhamiaji mbili, polisi nne, mahakama tatu, uchukuzi moja na mamlaka ya mapato Tanzania moja”.alieleza Mwakasege.

Alisema katika program ya Takukuru rafiki ambayo inatekelezwa kwa kushirikisha wadau katika ngazi ya kata ambapo wananchi hupata fursa ya kuibua kero zinazowakabili katika maeneo yao ambapo kwa kipindi cha Oktoba-Desemba walitembelea kata 11 na kupokea kero kuhusu sekta za elimu, afya, maji, fedha na nishati ambapo ufuatiliaji wake unaendelea.

Aidha alivitaja vipaumbele vya Takukuru kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka 2023/2024  ambavyo ni kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia vitendo vya rushwa,kutatua kero mbalimbali katika jamii kupitia programu ya Takukuru Rafiki na kuendelea kufuatilia rasilimali za umma kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha za umma.

Nyingine ni kufanya chambuzi za mifumo kwa lengo la kuzuia rushwa zinazosababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye mifumo ya utendaji wa sekta ya Umma na sekta binafsi ambapo amewahimiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha fedha zote za miradi zinatumika vizuri.