Miti yatajwa kuwa kinga dhidi ya joto kali

WATAFITI nchini Tanzania wamebaini ushahidi mpya unaoonyesha kuwa uwepo wa miti katika mashamba ya mazao yaani kilimo mseto (agroforestry) ni ulinzi thabiti dhidi ya hatari za kiafya zinazotokana na joto kali linaloongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti huo unaojulikana kama KISHADE (Kisiki Hai Sustainable Heat Adaptation Development) unaongozwa na LEAD Foundation kwa ushirikiano na London School of Hygiene and Tropical Medicine, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), na MetaMeta, kwa ufadhili wa Wellcome Trust.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Kiongozi wa Mradi kutoka LEAD Foundation, Dk Faraja Chiwanga, amesema hayo Oktoba 3, 2025, wakati wa Jukwaa la KISHADE (KISHADE Forum) lililofanyika sambamba na Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (Tanzania Health Summit) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa watafiti hao, kilimo mseto kina uwezo mkubwa wa kuboresha afya na mazingira ya kazi kwa mamilioni ya wakulima nchini sekta ambayo inachukua zaidi ya asilimia 70 ya nguvu kazi ya taifa.

“Lengo letu ni kujua kama kulima mazao pamoja na miti kunaweza kuleta tofauti katika afya za wakulima kwa kubadilisha mazingira yao ya karibu kazini,” amesema Dk Chiwanga.

Amebainisha kuwa wakulima wengi wanakabiliwa na magonjwa yanayohusiana na joto kama vile upungufu wa maji mwilini, shinikizo la damu, matatizo ya figo na mishipa ya damu, hasa kutokana na ukosefu wa kivuli na miundombinu ya kupunguza joto mashambani.

“Hatari hizi zimeongezeka kadiri joto linavyoongezeka, na miti inaweza kuwa suluhisho rahisi na la asili kwa kulinda afya ya wakulima,” ameongeza.

Watafiti walitumia teknolojia ya vitambuzi vinavyovaliwa (wearable sensors) kufuatilia joto la mwili na mapigo ya moyo ya wakulima kwa wakati halisi, sambamba na kuchukua sampuli za damu na mkojo ili kupima athari za kiafya zinazochangiwa na joto kali.

Kwa kulinganisha wakulima wanaofanya kazi katika mashamba yenye miti na wale wasio na miti, watafiti wameanza kuthibitisha kisayansi kwamba miti inapunguza joto la mazingira ya kazi na hivyo kulinda afya ya wakulima vijijini.

“Wakulima ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, lakini hawana ulinzi wa kutosha dhidi ya joto linaloongezeka kila mwaka. Tunataka ushahidi wa kisayansi uwe sehemu ya suluhisho,” amesema Dk Chiwanga.

Kwa mujibu wa LEAD Foundation, zaidi ya miti milioni 30 imepandwa na wakulima kupitia programu ya Kisiki Hai, hatua iliyosaidia kupunguza joto, kurejesha rutuba ya udongo na kuongeza ustahimilivu wa kilimo nchini.

“Tukiwekeza kwenye miti, tunalinda maisha. Hii si tu kuhusu mazingira, bali ni kuhusu afya ya binadamu na mustakabali wa kizazi kijacho,” amesisitiza Dk Chiwanga.

Kwa upande wake Dk Richard Sambaiga, Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Anthropolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mratibu wa Mradi wa KISHADE, amesema utafiti huo umefanikiwa kuwahusisha wananchi moja kwa moja.

“Timu ya utafiti imepokea ushirikiano mkubwa kutoka jamii, jambo lililowezesha ukusanyaji wa data za uhakika. Wakulima wameonyesha hamasa kubwa kutumia teknolojia kama sensa zinazovaliwa,” amesema Dk Sambaiga.

Utafiti huo pia unalenga kujenga uwezo wa ndani kwa kutoa mafunzo kwa kizazi kipya cha watafiti wa Kitanzania, kuhakikisha urithi wa kazi unaendelea hata baada ya mradi kukamilika.

Juma Mrisho kutoka taasisi inayojihusisha na utunzaji wa mazingira katika maeneo yasiyo na mvua nyingi, amesema wamezalisha zaidi ya miti milioni 30 katika ukanda wa kati, ili kuchunguza jinsi inavyosaidia mashamba kurekebisha hali ya hewa.

“Tunajua madhara ya joto kali katika mwili wa binadamu, lakini sasa tunataka kuangalia namna miti inavyosaidia mkulima kupunguza athari za kiafya zitokanazo na kufanya kazi kwenye jua kali,” amesema.

Ameongeza kuwa utafiti wao umebaini joto kali linaongeza hatari ya magonjwa yanayohusiana na upungufu wa maji mwilini, hivyo elimu na miongozo ya tahadhari inahitajika kwa wanaofanya kazi kwenye mazingira ya jua.

“Wakulima wanapaswa kubakisha baadhi ya miti mashambani mwao ili kusaidia hali ya hewa na kulinda afya zao. Mabadiliko ya tabianchi yanasababishwa zaidi na matendo ya binadamu,” ameongeza.

Alfredi Kandoya, mtaalamu wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), alisema wamekuwa wakitoa taarifa kwa wananchi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, hasa kuhusu unyevunyevu na joto la kila siku.

“Kuanzia Novemba hadi Aprili huwa ni msimu wa joto kali kuliko miezi mingine. Hali hii inaathiri uwezo wa watu kufanya kazi na pia kuharibu mazao mashambani,” amesema Kandoya.

Amesisitiza umuhimu wa wakulima kutumia taarifa hizo kupanga shughuli zao za kilimo, kupanda, kuvuna na hata kukabiliana na vipindi vya ukame.

Mkulima kutoka Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, amesema kabla ya mradi wa Kisiki Hai walikumbana na changamoto nyingi za ukosefu wa mvua, joto kali, na maradhi ya mara kwa mara.

“Tulikuwa tunaumwa kichwa, homa, na kupungukiwa na maji mwilini. Baada ya kupata elimu hii, tumepata mkombozi wa mazao yanapatikana na afya zetu zimeimarika,”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button