MKANDARASI wa Kampuni ya Palemon Construction Ltd ya jijini Mwanza anadaiwa kutelekeza tenda ya mradi wa barabara yenye urefu wa mita 300 iliyopo mtaa wa Molinge mjini Geita.
Meneja wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Geita, Mhandisi Japherson Nnko amethibitisha hilo mbele ya waandishi wa habari wakati akifafanua kukwama kwa mradi huo.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulitarajiwa kuanza Juni 6, 2022 na kukamilika Novemba 3,2022 kwa gharama ya Sh milioni 230 lakini mkandarasi hajakamilisha na ameshaondoka.
“Mradi haujaenda kama ulivyotarajiwa kwa sababu mpaka sasa muda umeisha kabisa, kwa maana ya muda tupo kama asilimia 115 lakini kazi iliyofanyika ni chini ya asilimia 10.” Amesema na kuongeza,
“Sisi mashariti yote ya mkataba kama mwajiri tumeshakamilisha ikiwemo malipo ya awali, na ameshalipwa takribani sh milioni 21 kama malipo ya awali kumsaidia kwa ajili ya kufanya kazi.”
Amesema ameshaandikiwa barua ya onyo na sasa anakatwa asilimia 0.01 kwa kila siku anavyochelewa kukamilisha mradi na endapo makato yatafikia asilimia 10 atavunjiwa mkataba kwa mjibu wa sheria.
“Tunaangalia pia vipengele vingine vya mkataba, ametakiwa kutuletea udhamini wa benki asipofanya sawa sawa, kwani ana benki ambayo imemudhamini, itawajibika.”
Mwenyekiti wa Mtaa wa Molinge, kata ya Buhalahala mjini Geita, Adrian Rwechungura ameeleza barabara hiyo ni muhimu kwani inaunganisha stendi kuu ya mabasi na soko kuu la mji wa Geita.
Amesema mkandarasi huyo amesababisha kero kubwa kwa wananchi, wanafunzi na wakazi wa eneo hilo kwani kazi pekee iliyofanyika ni kuichimba barabara na kisha kuondoa mitambo eneo la mradi.
Mariam James, mjasiliamali wa chakula eneo hilo amesema alichokifanya mkandarasi huyo ni uharibifu badala ya matengenezo kwani barabara hiyo kwa sasa yanatuama maji mengi na kutopitika mvua inaponyesha.