Mke wa Besigye azuiliwa kumuona mumewe siku ya Krismas

UGANDA : MKE wa mwanasiasa mkongwe nchini Uganda Kizza Besigye,Winnie Byanyima ameeleza masikitiko yake kufuatia kuzuiliwa kumuona mumewe ambaye yuko gerezani, siku ya Krismasi.
Besigye, mwenye umri wa miaka 68, alikamatwa na kushtakiwa na mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki bastola na kujaribu kununua silaha nje ya nchi, tuhuma ambazo amezikanusha.
Kwa mujibu wa sheria za magereza nchini Uganda, wafungwa wote wanazuiliwa kutembelewa na familia zao au marafiki zao wakati wa sikukuu za Krismasi.
Hata hivyo, Winnie Byanyima, ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na VVU na Ukimwi, amesema kuwa atafanya kila liwezekanalo ili aweze kumuona mumewe.
“Siachi chakula cha Besigye langoni kama nilivyoelekezwa. Nitaenda huko na kumuona mume wangu kwa sababu siwaamini hata siku moja,” alisema Bi. Byanyima.
“Labda nitachukua hema na kulala huko… ikiwa ndivyo wanataka,” aliongeza, akieleza kukataa kukata tamaa kuhusu kumuona mumewe.
Besigye, ambaye amekuwa akigombea urais mara kadhaa dhidi ya Rais Yoweri Museveni, amekuwa mpinzani mkuu wa Rais Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.
Ingawa alishindwa katika chaguzi nne za urais, Besigye amekuwa na sauti kubwa katika siasa za upinzani nchini Uganda. SOMA: Besigye afikishwa mahakama ya jeshi
Katika miaka ya hivi karibuni, alijitenga na siasa na katika uchaguzi wa 2021 hakugombea.
Besigye alirudi kwenye vichwa vya habari mwezi uliopita baada ya kutekwa nyara akiwa ziarani nchini Kenya, kisha kupelekwa kwa nguvu Uganda na kufunguliwa mashtaka pamoja na msaidizi wake, Obeid Lutale.



