Mkenda ameitaka TIRA kuvutia wawekezaji

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuendelea kuweka miundombinu itakayovutia wawekezaji wengi zaidi wa sekta ya bima.

Amesema hayo leo jijini Mbeya kwenye uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Tanzania baada ya kutembelea banda la taasisi hiyo huku pia, akisifu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa taifa.

Advertisement

“Sekta ya bima mbali ya kusaidia kukinga majanga mbalimbali yanayotokea lakini pia ni sekta ambayo watanzania wanapaswa kutumia fursa iliyopo ili kuwekeza kwa kufungua kampuni na kujiingizia kipato binafsi na taifa kwa ujumla,”amesema.

Akijibu swali kuhusu njia zinazofanywa na mamlaka hiyo ili kuvutia uwekezaji kwa wazawa, mwanasheria Jamal Mwasha ambaye ni msajili wa migogoro ya bima katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima amesema Sheria ya bima sura ya 394 kupitia kifungu cha 16 imeweka sharti kuwa kila kampuni inayoanzishwa nchini, lazima walau theluthi moja imilikiwe na wazawa.

“Kwa hiyo Mamlaka ina hakikisha kifungu hiki kinazingatiwa ipasavyo na sharti hilo linatimizwa,”

Amesema pia mamlaka inatumia majukwaa mbalimbali inapokutana na wawekezaji na wadau wa sekta nyingine kuwapa elimu juu ya fursa zilizopo na kumekua na mwitikio mzuri.

Mwasha ameongeza kuwa mamlaka inasaidia uanzishwaji wa konsotia ya bima ya kilimo ambapo ni muunganiko wa kampuni wazawa walioweka mtaji ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wa skimu ya taifa ya bima ya kilimo na kuongeza uwezo wa kimtaji wa soko la bima nchini kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo.

Awali akimkaribisha waziri kwenye banda hilo Meneja Uhusiano na Mawasiliano Hadija Maulid ameeleza kuwa TIRA inashiriki kwenye maonesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha pamoja na wadau wa kampuni za bima kwa lengo la kutoa elimu kwa umma wa Tanzania kuhusu umuhimu bima lakini kwa kampuni zinazoshiriki zinatoa huduma za moja kwa wananchi wanaohitaji kukata bima mbalimbali.

Maonesho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa yafanyika jijni Mbeya katika viwanja vya Ruanda Nzovwe yalianza rasmi Oktoba 21 na yatahimishwa Octoba 26, 2024.