Mkurugenzi jiji Arusha, wenzake waongezewa mashtaka
MKURUGENZI wa Jiji la Arusha ambaye na wenzake wawili walikuwa wakikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la uhujumu uchumi, sasa wana mashtaka tisa baada ya Jamhuri kuongeza mashtaka mawili.
Dk John Pima alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwezi Mei mwaka huu hata hivyo siku chache baadaye alipandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Katika kesi namba tano ya uhujumu uchumi ambayo imeanza kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Dk. Pima na wenzake pia wamebadilishiwa Hakimu. Awali kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Fadhil Mbelwa hata hivyo mabadiliko mapya yaliyotangazwa Mahakamani hapo, kesi hiyo sasa itasikilizwa na Seraphin Nsana.
Upande wa Jamhuri umepanga kutumia mashahidi 28 akiwemo Mkuu wa Utawala jiji la Arusha, Gerald Nyehomungare na vielelezo 37. Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwekahazina wa Jiji la Arusha Mariam Mshana na Mchumi wa Jiji hilo, Innocent Maduhu.
Akitoa ushahidi, Nyehomungare alidai kuwa mbali na kuwa Katibu wa Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji hilo (CMT) hakuwahi kuona taarifa ama tuhuma dhidi ya watuhumiwa hadi zilipoibuliwa na Waziri Mkuu Mei 25 mwaka huu.
Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili sita ambao ni pamoja wakili Patrick Mwita, Monica kijazi, Nyasonga Christopher na Timotheo Malya huku mawakili wanne Mpaya Kamara Edmund Ngemela, Mosses Mahuna na wakili Sabato Ngogo wakiwa upande wa utetezi.
Kesi hiyo inaendelea leo Novemba 10 kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri.