Mkutano wa kikanda matumizi ya nishati waanza Arusha

MKUTANO wa kikanda wa matumizi bora ya nishati unaojumuisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza kwa mafanikio kwa kuonesha teknolojia mbalimbali za matumizi bora ya nishati ikiwemo majiko na magari.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amekagua mabanda ya maonesho ya wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mkutano huo ulioanza jijini Arusha ambao utafunguliwa leo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Pamoja na kukagua mabanda hayo ya maonesho, Dk Mataragio alikagua shughuli nyingine zinazoendelea kukamilishwa kuelekea siku ya ufunguzi rasmi wa mkutano huo.

Katika Mabanda ya Maonesho, Dk Mataragio alijionea vifaa mbalimbali vinavyotumia umeme kidogo ikiwemo majiko, brenda, mashine za kusukuma maji na magari ya umeme.
Dk Mataragio amesema kupitia REEC 2024, Tanzania inataka kutoa ujumbe wa jinsi inavyojikita katika jitihada za kupunguza hewa ya ukaa kwa kutumia vifaa vya nishati visivyochafua mazingira.
“ Katika Maonesho haya nimeona kuna majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo na gharama ndogo kuivisha chakula, nimeona majiko ambayo yanaweza kuivisha maharage kwa gharama ya Sh 300 tu ambayo ni chini ya unit moja ya umeme wakati ukitumia mkaa utahitaji Sh 3000 hadi 4000,” amesema Dk Mataragio.




