Mlalamikaji kumhudumia mahabusu ni kulea uhalifu

Charles Mwijage

JANA katika kikao cha mkutano wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma, serikali imezungumzia vitendo vya mlalamikaji kulazimishwa kugharimia usafi rishaji wa watuhumiwa au mahabusu kwenda na kurudi rumande.

Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage kupitia swali lake bungeni kabla ya kujibiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini. Mbunge huyo alihoji sababu za mlalamikaji kulazimishwa kumgharimia mahabusu, kwa kutaja Tarafa ya Kamachumu, wilayani Muleba katika Mkoa wa Kagera kuwa ndipo vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika.

Akijibu, Sagini aliamuru vitendo hivyo viachwe mara moja huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na kanuni zilizopo. Ufafanuzi wa naibu waziri uliweka bayana kwamba sheria na kanuni zinaeleza wazi kuwa utaratibu wa kuwasafirisha watuhumiwa au mahabusu hutekelezwa na Jeshi la Polisi.

Advertisement

Sheria hiyo ni ya Polisi, Sura ya 322 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na Kanuni 353 na 354 ya Kanuni ya Jeshi la Polisi zinazosimamia watuhumiwa au mahabusu walioko kwenye vituo vya polisi.

Sagini alisisitiza kuwa jukumu la kuwasafirisha watuhumiwa au mahabusu kutoka rumande gerezani kwenda mahakamani ni jukumu la Jeshi la Magereza kwa mujibu wa Kifungu cha 75 cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Tunampongeza mbunge aliyewasilisha suala hili mbele ya mhimili wa Bunge na wakati huohuo serikali kutoa majibu na ufafanuzi unaoweka bayana kwamba vitendo hivyo si sahihi kufanyika. Alichosema mbunge si cha jimboni kwake pekee, bali katika maeneo mengi hususani vijijini. Wananchi wamejikuta wakisita kufuatilia watu waliowatendea uhalifu kutokana na kuepuka ama usumbufu au gharama za kuwahudumia pale wanapokamatwa na vyombo vya usalama.

Baadhi ya watu wamejikuta ‘wakiwasamehe’ bila kupenda watu waliowafanyia uhalifu wa aina mbalimbali kutokana na kutokuwa na fedha au kukwepa kuingia gharama. Katika baadhi ya maeneo, licha ya kutakiwa kumgharimia mtuhumiwa, walalamikaji wamekuwa wakibanwa pia kuwagharimia nauli pia mgambo au askari.

Fikiria, mtu aliyeibiwa analazimika kumlipa posho mgambo na nauli ya kwenda kumfikisha mtuhumiwa kituo cha polisi na wakati mwingine anatakiwa pia kumlipia chakula! Hii si sawa. Vitendo hivi ni kikwazo katika kupambana na vitendo vya kihalifu.

Ukiacha wale wanaoweza kuamua kuachana na kesi kwa kuhofu gharama, wapo wale wanaoweza kuamua kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa kabla ya kuwafikisha kwenye mamlaka zinazohusika kwa kuepuka adha kama hizo.

Tunapongeza kauli ya serikali kwamba, wizara imefanya mawasiliano na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) ili wawaelekeze wasaidizi wao ngazi za mikoa na wilaya kuzingatia sheria.

Tunashauri suala hili lifuatiliwe kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa kuhakikisha walalamikaji hawatwishwi mzigo wa kuhudumia watuhumiwa; badala yake, wapate kwa mujibu wa sheria. Kama tatizo ni bajeti, basi ni vyema iongezwe kwa ajili hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *