Mmoja afa, kaya 150 zaathirika mafuriko Kilosa

MOROGORO; KAYA zaidi ya 150 zimekosa makazi kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na Mto Wami, ambapo mtu mmoja mwanaume mkazi wa Rudewa wilayani Kilosa amefariki dunia alipokuwa akijaribu kujiokoa kutokana na mafuriko hayo.

Mafuriko hayo yanatokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, ambapo Mto Wami umejaa maji na kusababisha kubadili uelekeo wake wa wakawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, akizungumza kwa simu leo Desemba 5, 2023 amesema baada ya maji kujaa kwenye Mto Wami, yalipoteza uelekeo wake na kusababaisha mafuriko na nyumba kadhaa kuzingirwa na maji, nyingine kubomoka na kusababisha kaya zaidi ya 150 kukosa makazi.

“ Kifo cha mwanaume huyo kimetokea kati ya saa 11 na 12 asubuhi ya Desemba 5, mwaka huu baada ya yeye na mkewe wakijaribu kuvuka maji kwa nia ya kujiokoa.

“Maji yalimzidi nguvu mwanaume huyo na kupoteza maisha , mwili wake kwa bahati nzuri uliokotwa ukiwa unaelea kwenye maji,” amesema Shaka.

Amesema maji mengi yaliyojaa Mto Wami yamechangiwa na mvua zinazonyesha mikoa ya Manyara, Dodoma na Singida na yalishindwa kufuata mkondo sahihi, hivyo kupoteza uelekeo na kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Amefafanua kuwa baadhi ya nyumba zimebomoka kutokana na maji mengi ya mvua kupita kwa kasi na kupasua kingo ndogo za mto Mkondoa, pamoja na mto Wami na hivyo kuleta madhara katika eneo la Rudewa na Mvumi.

“ Uongozi wa wilaya kwa sasa kipaumbele ni kuwasaidia watu kutoka kwenye maji, ili kusitokee madhara zaidi na kuwahifadhi maeneo salama ,”amesema Shaka.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button