DAR ES SALAAM: Katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani Taasisi ya Tiba ya Mifupa na ubongo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) imeendesha bure kambi maalumu ya uchunguzi wa mifupa kwa watoto ambapo watoto zaidi ya 100 wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Daktari bingwa mbobezi wa mifupa uti wa mgongo na majeruhi na Mkurugenzi wa upasuaji wa mifupa na tiba ya majeraha wa Taasisi hiyo, Dr Anthony Assey amesema lengo la kambi hiyo ni kusaidia watoto na wazazi kugundua mapema matatizo ya viungo ili kuyatatua mapema.
“Tumegundua watoto wengi wanafika hapa wamechelewa tangu wazazi waone matatizo haya na kibaya zaidi ni watoto wa hapahapa Dar es Salaam au maeneo ya jirani kwa hiyo tukaona kuna haja ya kuwaita kwenye kambi ambayo sio kama kuja hospitali kawaida ili kugundua matatizo haya mapema” amesema Dr Assey
Kwa upande wake Daktari bingwa mbobezi wa mifupa na viungo kwa watoto Dr Bryson Mcharo ameeleza matatizo ambayo yameonekana kwa wingi katika kambi hiyo.
“Tulikuwa na wasiwasi hawa wagonjwa wanaenda wapi kwa hiyo magonjwa ambayo yameonekana kwa wingi ni magonjwa ya watoto ambao wana mtindio wa ubongo lakini wana changamoto za mifupa kama vile nyonga kuchomoka, kuna ambao wamezaliwa baadhi ya viungo vyao haviko sawa, lakini pia wapo watoto ambao wanakuja upande mmoja wa mguu ni mkubwa kuliko mwingine lakini wengi kabisa ni wagonjwa wenye matege”
Kambi hiyo ya Matibabu hayo itadumu kwa siku moja na inatarajia kufikia watoto zaidi ya 200.