MOI yazindua mpya wa kuweka miadi

DAR ES SALAAM: Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imezindua mfumo maalumu wa kuweka miadi na madaktari ujulikanao “MOI Online appointment system “ ambao utamuwezesha mgonjwa kuweka miadi ya kuonana na daktari anayemtaka bila kufika MOI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI, Balozi Dk Mpoki Ulisubisya amezinduzi mfumo huo Septemba, 15, 2025 huku akidai mfumo utaondosha usumbufu na msongamano wa wagonjwa wanaofika kuweka miadi kuonana na daktari.
“Kupitia mfumo huu, mgonjwa ataweza kumchagua daktari anayemtaka, siku na muda wa kumuona na kliniki anayohitaji, utaondoa usumbufu wa wagonjwa kufika kliniki na kisha kuambiwa hiyo kliniki kwa leo haipo au daktari husika ana udhuru…wagonjwa hawatalazimika kufika mapema kwa ajili ya kuweka foleni ya kumuona daktari,” amesema Dk Mpoki.
Dk Mpoki amesema mgonjwa baada ya kufanya miadi atapokea ujumbe mfupi wa simu ukimtaarifu kukubalika kwa miadi yake. Aidha mfumo huo unapatikana saa 24/7 kwa kutumia simu janja, kompyuta mpakato au kishikwambi kupitia tovuti kuu ya taasisi https://www.moi.ac.tz.
Ametoa wito kwa Watanzania kuanza kutumia mfumo huo kwa ajili ya kuweka miadi kwa madaktari wa taasisi ya MOI ili kufanikisha adhima ya kutoa huduma za kidigitali katika kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.



