Mpango aiita Korea fursa za uwekezaji

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Tanzania inathamini na imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Korea ulioanza tangu mwaka 1992.
Dk Mpango amesema hayo katika Ikulu ya Chamwino Dodoma alipokutana na kuzungumza na Balozi wa Jamhuri
ya Korea nchini, Eunju Ahn.

Ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya elimu, miundombinu, Tehama, afya,
kilimo, viwanda na nishati.
Dk Mpango alisema makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Korea katika madini ya kimkakati, yataleta
manufaa mengi zaidi kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini yanayoenda sambamba na mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo inajikita katika uchumi wa teknolojia za kijani.

Alieleza umuhimu wa kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Korea yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Dk Mpango alisema ni muhimu wawekezaji na wafanyabiashara wa Korea watembelee Tanzania mara kwa mara ili kujionea fursa zilizopo na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali, ikiwamo ya viwanda.
Amesema uongezaji wa thamani kwa malighafi nchini utachochea biashara, uhamishaji teknolojia pamoja ongezeko la ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Pia, alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Jamhuri ya Korea katika kubadilishana wafanyakazi na akamsihi, Balozi huyo kuwezesha mchakato wa kujiunga katika Mfumo wa Vibali vya Ajira (EPS) ili wafanyakazi wa Tanzania waingie katika soko la ajira la Korea na kufanya kazi katika sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa meli, sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa.
Alisema ushirikiano unahitajika katika elimu na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kwa kuwapatia mafunzo katika ubingwa na ubobezi wa utoaji matibabu mbalimbali.
Pia, alihimiza ushirikiano katika utamaduni, michezo na Lugha ya Kiswahili.
Balozi Ahn alisema katika kipindi atakachohudumu nafasi ya ubalozi nchini Tanzania, atasimamia na kuharakisha
kukamilika kwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, ikiwamo ushirikiano
katika madini ya kimkakati na maendeleo ya uchumi wa buluu.



