Mpango ataka habari za utu

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameonya dhidi ya uandishi wa habari usiozingatia maadili, utu na heshima, akisisitiza baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kusambaza taarifa zinazodhalilisha na kuumiza wengine bila kujali athari zake kwa jamii.

Dk Mpango alitoa onyo hilo wakati wa kufunga Mkutano wa 109 wa mwaka wa Watayarishaji wa Vipindi vya Elimu kwa Umma uliofanyika mkoani Mbeya.

Alisisitiza sekta ya habari inapaswa kuzingatia maadili, sheria na mila za Kitanzania, kulinda heshima na utu wa kila mmoja.

Aidha, alitoa wito kwa waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma kuwekeza katika kukuza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Alihimiza vyombo vya habari kujikita katika kampeni za usafi na utunzaji wa mazingira badala ya kusubiri matukio mabaya kama milipuko ya magonjwa, moto kwenye misitu au mafuriko ndipo viweke uzito katika kuripoti masuala hayo.

Aliwataka waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma kujifunza zaidi na kutoa elimu sahihi kuhusu maendeleo ya
sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya Akili Mnemba, roboti na usalama wa mitandao.

Aliwataka waandaaji hao kutumia Kiswahili sanifu na fasaha na kuwa mabalozi wa lugha hiyo ndani na nje ya nchi.

Aliwaasa washiriki wa mkutano huo kujiepusha na uandishi wa habari unaoibua taharuki na migogoro kwa taifa.

Alisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa zinazogusa maslahi ya wananchi, hususani elimu ya uraia na uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akiwakumbusha Watanzania kulinda amani na utulivu wa nchi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, usikivu wa redio ya taifa umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2016 hadi asilimia 87 mwaka 2024.

Alitoa wito kwa wadau wa elimu kwa umma kutumia usikivu wa redio kutangaza shughuli zinazofanywa na serikali.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayub Rioba alisema kauli mbiu ya mwaka
huu ambayo ni ‘Tumia nishati safi na Tunza mazingira’ inaenda sambamba na vipaumbele vinavyosimamiwa na
serikali.

Alisema TBC imechukua suala la nishati safi na usafi wa mazingira kwa umuhimu mkubwa kwa kutambua suala hilo lina maslahi kwa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button