Mpango: Samia amedhihirisha anaimudu vizuri kazi ya urais

DODOMA : MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amedhihirisha anaimudu vizuri kazi ya urais.

Dk Mpango alisema hayo wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea wa urais wa CCM, Rais Samia mjini Dodoma . Alisema CCM haiwezi kubabaisha kupeleka mtu wasiyemjua kama mgombea wa nafasi hiyo. “Naomba niwaambie wanaCCM wenzangu na Watanzania wote, kazi ya urais hatuwezi kubabaisha kupeleka mtu tusiyemjua, Mama Samia amedhihirisha kwamba anaimudu vizuri mno,” alisema Dk Mpango.

Alisema katika maeneo ambayo amekuwa akienda kwa kutumwa na Rais Samia, ana heshima kubwa na wanatamani awe ndiye rais wao kwa namna ambavyo si mtu wa kubabaisha. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alisema tangu Tanzania ianze kuwa na uhuru wa kuchagua rais kuna mikoa miwili ambayo imekuwa na rekodi nzuri ambayo ni Iringa na Dodoma.

“Rekodi za huko nyuma zinaonesha kwamba kila mara tumekuwa tunawapa marais wetu wagombea kura nyingi kuliko mikoa mingine katika jamhuri yetu sasa nawaomba safari hii ndugu zangu wote wa mkoa wa Dodoma, mimi nina uhakika wananchi wote wa Dodoma tutampa kura zetu Dk Samia,” alisema Malecela. Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Bashiru Ally alisema tangu Samia alipozindua kampeni aliwaelekeza wanachama na viongozi wa chama katika ngazi zote kuweka msisitizo katika ubora wa wagombea.

“Tutapita kila mahala nyumba kwa nyumba, shina kwa shina, tawi kwa tawi, kata kwa kata, tarafa kwa tarafa, wilaya kwa wilaya, kitanda kwa kitanda katika ngazi zote urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar, Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Madiwani,” alieleza Bashiru. Alimhakikishia Samia kwamba mwaka huu ushindi utakuwa mkubwa kuliko wakati mwingine wowote wa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi na sababu ni kwamba wamesimamisha wagombea bora.

“Kazi nyingine uliyotupa ni kutetea rekodi ya utendaji wa chama chetu kwa miaka mitano iliyopita, kazi tulizozifanya na ahadi tulizozitoa mwaka 2020 na kazi ya tatu ni kufafanua yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika ngazi ya taifa, mkoa na wilaya,” alisema Bashiru.

Alisema mwaka huu Halmashauri Kuu ya CCM imetengeneza kanda 11 nchi nzima. “Na mimi nimekuwa na bahati ya kuwa sehemu ya waratibu katika kanda hizo 11, kanda yetu mimi na Dk Mpango ni Dodoma, Singida na Tabora na wakati tutakapokuwa tukifanya tathmini baada ya uchaguzi, kanda hii itaibuka kidedea ikiwa namba moja,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button