Mpina aenguliwa kugombea urais

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa Luhaga Mpina kugombea urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ilithibitisha kwamba wamepokea taarifa ya uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kubatilisha uteuzi wa Mpina kugombea urais kupitia chama hicho.
Uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa umetokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala akipinga uhalali wa mchakato wa uteuzi wa Mpina.
Chama hicho kupitia taarifa yake, kimepinga uamuzi huo kikisema kitafungua kesi Mahakama Kuu.
Shaibu alisema mchakato wa uchaguzi ulishaanza na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa fomu na wagombea wanaendelea na taratibu za ujazaji na urejeshaji wa fomu.
Alieleza kwamba mgombea wao amezunguka nchi nzima kuomba udhamini, amekula kiapo mahakamani na amekamilisha taratibu zinazohusu ukamilishaji wa fomu za kugombea urais.
Awali, HabariLEO ilipompigia Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kufahamu zaidi juu ya uamuzi alisema: “Uamuzi umetolewa, waulize ACT…”
Katika malalamiko ya mwanachama huyo wa ACT Wazalendo aliyowasilisha kwa Ofisi ya Msaljili wa Vyama vya Siasa, alidai kwamba chama hicho kilikiuka kanuni na sheria za uteuzi wa mgombea.
Alidai kwamba Katibu Mkuu wa chama hicho alipuuza kanuni za kudumu za chama hicho za mwaka 2015, hasa kifungu 16 (4) (i), (iii) na (iv) ambacho kinamtaka mgombea wa urais kuwa mwanachama angalau mwezi mmoja kabla ya mwisho wa uteuzi.
Alidai Mpina hakuwa mwanachama kwa kipindi kinachohitajika, akirejelea kifungu 4 (8) (a) kinachotaka mwanachama awe ndani ya chama si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa madai hayo, Mpina alijiunga na ACT Wazalendo Julai 28, mwaka huu nje ya muda wa mchakato wa uchaguzi uliokuwa kati ya Januari 15 na Mei 25 mwaka huu.
Awali, Mpina alichukua fomu kuomba kugombea ubunge Jimbo la Kisesa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini chama hicho hakikumpitisha.