Mradi ujenzi njia ya umeme Mtwara Mjini -Tandahimba waiva

MTWARA; Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) nchini imekabidhiwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovot 33 kutoka Mtwara mjini mpaka Tandahimba mkoani Mtwara.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Abdul Mihambo amesema mradi huo wenye urefu wa kilometa 92.3 umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme Wilaya ya Tandahimba na Nanyamba, Mtwara.
“Utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha miundombinu ya umeme na kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.

Mihambo amesema hayo wakati wa ziara ya kumtambulisha mkandarasi wa mradi huo EDTCO kwa viongozi wa Wilaya ya Tandahimba na Nanyamba.
Amesema TANESCO watashirikiana na EDTCO kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia viwanga vinavyotakiwa.
Meneja Mkuu wa EDTCO, Mhandisi Richard Mwanja amesema kuwa mradi huo ambao unatarajiwa kumalizika ndani ya mwaka mmoja utekelezaji wake umeanza kwa kusimika nguzo za umeme.
“Kutokana na kasi ya kazi tuliyoanza nayo tunatarajia kumaliza ujenzi wa mradi kabla ya mwaka uliopangwa,’ amesema na kuomba ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo.



