Mradi wa barabara Kyema-Katerero wafikia 80%
MRADI wa barabara ya lami Kyema – Katerero iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera unaotekelezwa kwa awamu ya tatu chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tarura, wenye urefu wa kilomita 0.5 umefikia asilimia 80.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Tarura Wilaya ya Bukoba, Andondile Mwakitalu amesema utekelezaji wa mradi huo awamu ya tatu ulianza Septemba 15, 2023 unatarajia kukamilika Oktoba 15, 2024 kwa gharama za Sh milioni 223.
Ameongeza kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 80 na ukikamilika utasaidia kurahisisha wananchi kupata huduma za kiafya hospitali ya wilaya pamoja na kufika kwa wepesi ofisi za halmashauri.
“Hadi sasa mradi umefikia asilimia 80, faida za mradi huu ni kurahisisha ufikaji wa wananchi Hospitali ya Wilaya na ofisi za Halmashauri ya wilaya na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa wananchi wa kata ya Kemondo na Katerero”.
Baadhi ya watumiaji wa barabara hiyo wamesema kuwa awali walikuwa wakitesema kupata huduma za afya kutokana na umbali na ubovu wa barabara hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yao ila kwa sasa mwarobaini umepatikana.
“Kuja kwa hii barabara kwetu imeonekana ni fursa maana kipindi cha nyuma tulikuwa tunateseka kutokana na ubovu wa barabara wakati wa kwenda kupata huduma za afya na kusafiri,” amesema Yurida Augustine.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Jason Rweikiza amesema kuwa barabara hiyo ambayo ujenzi bado unaendelea ni kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania hususani wakazi wa kata hizo.
“Kwenye kuboresha maisha ya Mtanzania wa Bukoba vijijini, ujenzi unaendelea na hivi karibuni pia utaanza utekelezaji wa mradi wa barabara kiwango cha lami kuanzia Kyetema mpaka Kyaka”. amesema Rweikiza.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava baada ya kutembelea na kukagua mradi huo wa barabara ameridhishwa na utekelezaji wake.