Mradi wa maji wa bil 12.8/-wazinduliwa Lamadi

RAIS Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Simiyu kwa kuzindua mradi mkubwa wa maji Lamadi ambao umegharimu Sh bilioni 12.8.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri alisema mradi huo umelenga kuwahudumia wananchi 85,000.

Alisema wananchi hao ni kutoka katika vijiji vya Lutubiga, Lamadi pamoja na Mkula, huku akibainisha kuwa chanzo chake kina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni nne kwa siku.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema wananchi wa Lamadi walipata maji kwa asilimi 23, ambapo baada ya kujengwa kwa maji kiwango cha upatikanaji wa huduma hiyo kimepanda hadi kufikia asilimia 97.

“Rais (Samia) umebeba ajenda ya maji na kufanikiwa kumtua mama ndoo kichwani, uwepo wa mradi huu umedhihirisha dhamira yako ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama,” alisema.

Alisema wananchi wa Lamadi, Mkula pamoja na Lutubiga wanapata huduma ya maji muda wote. Alimshukuru Rais Samia kwa kubadilisha wizara hiyo kutoka wizara ya kero na shida na kuwa wizara ya furaha.

Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Rais Samia alimshukuru waziri pamoja na watalaamu wa wizara hiyo kwa kusimamia mradi huo hadi kukamilika na wananchi kuanza kupata maji safi na salama.

“Nilikuwa naongea na Waziri (Aweso) akaniambia sasa wananchi wa Lamadi wanapata maji kwa asilimia 97 baada ya mradi huu, hongereni sana na hizo asilimia tatu ambazo zimebaki tunakwenda kuzimaliza,” alisema.

Rais Samia alisema serikali imejipanga kuhakikisha maisha ya Watanzania yanastawi kwa kupata huduma bora za kijamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

“Serikali ipo kuhakikisha maendeleo yenu wananchi yanapatikana, ustawi wa afya zenu na ustawi wa familia unaonekana na ndiyo maana tumejitahidi huduma zote za kijamii zinapatikana, kama elimu, maji pamoja na afya,” alisema.

Rais Samia alisema kutokana na serikali kuboresha huduma zote za kijamii ni wakati wa wananchi kufanya kazi kwa nguvu na kuongeza uzalishaji ili kukuza uchumi wao wenyewe na taifa kwa ujumla.

Aliwataka wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili familia na jamii zipate nguvu zaidi zifanye maendeleo zaidi.

“Kwa kuwa serikali imeboresha afya, elimu, huduma za maji, ni wakati sasa wa wananchi kufanya kazi kwa nguvu zaidi, kuzalisha mazao ya chakula, mazao ya biashara ili familia zetu ziweze kupata maendeleo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, utulivu ili serikali iweze kufanya kazi kubwa zaidi ya kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Alisema kuwa maendeleo yanayoonekana yanatokana na amani na utulivu ambao umeendelea kuwepo nchini, ikiwemo utulivu wa kisiasa pamoja na uwezo wa serikali kukusanya kodi na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button