Mrithi wa Kinana kupatikana Jan 19

DODOMA; MKUTANO Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatarajia kufanyika Januari 18 na 19 mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na kazi ya kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Abdulrahman Kinana ambaye aliomba kupumzika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema mkutano mkuu huo utakuwa na ajenda tatu.

Nazo ni kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, kupokea kazi za chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alieleza kuwa taarifa hizo za utekelezaji ilani ni kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Kuhusu mchakato wa kujaza nafasi iliyoachwa na Kinana, alisema mrithi wa nafasi hiyo anatarajiwa kupatikana baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM itakayokutana Januari 16 na kuja na mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Halmashauri Kuu ya CCM.

Alisema mapendekezo hayo yatafikishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ambayo itawasilisha jina hilo kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura ya ndio au hapana.

“Kumekuwa na uvumi, unaona vichwa vya habari kwamba CCM patashika, wafuatao watajwa kurithi nafasi ya Kinana, nani kati ya hawa atachukua nafasi ya Kinana, wengine wanakwenda mbali kuandika wafuatao kuchukua nafasi ya Kinana. Kila mmoja anaandika anavyotaka. Nataka kusema kwamba, nafasi ya Makamu Mwenyekiti haigombewi, unaposema kinyang’anyiro kinatoka wapi wakati nafasi haigombewi wala haijazwi fomu,” alisema.

Makalla alisisitiza, “Tutampata makamu mwenyekiti baada ya mapendekezo ya kamati kuu na halmashauri kuu, kisha jina la atakayeziba nafasi hiyo litawasilishwa katika mkutano mkuu na hapo ndipo zitapigwa kura ya ndiyo au hapana.”

“Hatukuwa kimya, chama kinaongozwa kwa katiba, kina utaratibu wake, hatuwezi kuongozwa kwa hisia za watu. Kwa sasa Kamati Kuu imeona ndiyo muda mwafaka kujaza nafasi hiyo,” alisema.

Makalla alibainisha kuwa mkutano mkuu utatanguliwa na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM vinavyotarajiwa kufanyika Januari 16, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button