Msajili ataka wanasiasa watii sheria

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewataka viongozi wa vyama hivyo kutii sheria za nchi na kusisitiza ofisi hiyo haihusiki kumtetea kiongozi yeyote atakayevunja sheria.
Hayo yalisemwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ali Ahmed (pichani) akitoa mada kuhusu Nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika Kukuza Demokrasia hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza hayo Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoshirikisha mdahalo wa amani uliohusisha viongozi wa dini na wadau wengine kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mdahalo huo uliandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania.
Ahmed alisema walikubaliana na vyama vya siasa kwenda kwenye uchaguzi huo wakiwa wamoja. “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tuna ushirikiano na vyama vya siasa na tumekuwa tukikutana mara kwa mara na hata katika maandalizi ya uchaguzi huu, tulikutana pale Dodoma pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na vyama vyote vikapewa orodha ya wapigakura,” alisema Ahmed.
Alisema ushirikiano huo upo na umekuwepo hata kabla ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na kuwa wanashirikiana na vyama hivyo kupitia viongozi wao kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi na tume imekuwa sikivu.
Hata hivyo, alitahadharisha viongozi wa vyama vya siasa kuwa ofisi hiyo haihusiki na kiongozi wa chama anayevunja sheria za nchi kwa sababu ziko mamlaka zinazomwajibisha yeyote akayetenda jinai na makosa mengine kwa mujibu wa sheria.
“Ofisi ya msajili inashughulika na masuala ya siasa haihusiki na wanasiasa wanaovunja sheria za nchi kwa kigezo cha kudhani ofisi hiyo itawasaidia, endapo mwanasiasa atavunja sheria za nchi, atashughulikiwa na vyombo husika kwa mujibu wa sheria, hivyo tuwatake wanasiasa wazingatie na kutii sheria za nchi,” alisema Ahmed.
Alisema ndiyo sababu wanakumbushana kudumisha demokrasia na kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria za nchi na kuepuka kutenda makosa ya jinai na mengine.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Hamza Hassan Juma aliwataka Watanzania walinde amani na kamwe wasikubali kuivunja.
Akimwakilisha mgeni rasmi, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, Juma alisema amani ya Tanzania ni uti wa mgongo kwa nchi za Afrika Mashariki na kati. “Amani ikitetereka Tanzania itakuwa shida, kuna mifano mingi ambayo nchi zilikuwa moja ila kutokana na imani na itikadi tofauti, wakaivunja na leo wengi wanaitwa wakimbizi, wengine walipata ulemavu wa kudumu na bado baadhi wanaendelea kupambana wenyewe kwa wenyewe,” alisema Juma.
Hivyo akawataka Watanzania kuondoa tofauti zao na kuendeleza umoja kwa kushirikiana kwa sababu amani iliyopo iliwekwa wa waasisi wa taifa ambao nao licha ya kuwa na itikadi tofauti za dini walikuwa wamoja na kuilinda amani.
“Endapo waasisi hao wangeangalia itikadi za dini zao, Mwalimu Julius Nyerere (Mkristo) na Shehe Abeid Amani Karume (Muislamu) wakatengana, umoja na muungano wa nchi usingepatikana. SOMA: Uchaguzi Mkuu 2025 kielelezo cha demokrasia EAC
Hivyo, kuungana kwao bila kujali imani ya dini zao ni jambo kubwa la msingi linalopaswa kuenziwa,” alisema Juma. Alisema kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaamka na jambo au mambo yao ambayo hawakuwashirikisha viongozi wenzao ndani ya chama husika na kulitoa kwa wananchi na kuzua taharuki na kusema jambo hilo ni baya na linaweza kuleta athari katika jamii.
Alihimiza Watanzania walinde umoja na amani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu ili kuendeleza misingi imara ya umoja wa taifa kwani uchaguzi utapita na taifa linapaswa kuendelea kuwa na umoja.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Amani nchini, Alhad Mussa Salum alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu kuendeleza amani na kutojihusisha na vitendo vinavyochochea ubaguzi.
Aidha, alisema makundi muhimu katika jamii likiwemo la vijana, wanawake na wenye ulemavu yanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu na sera jumuishi ili washiriki kikamilifu katika mchakato huo.



