Msako wasiofuata sheria uuzaji vyakula vya mifugo waja

MSAKO wa kuwashughulikia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo wasiofuata sheria na kanuni zinazoongoza utekelezaji wa shughuli hizo kuanza.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari ( TVLA), IMikiyoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Stella Bitanyi ameisema hayo alipotoa taarifa ya yaliyobainika wakati wa operesheni maalum iliyoendeshwa na timu ya wataalam kutoka ofisini kwake kwa kushirikiana na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka wizarani.

Timu hiyo ilifanya ukaguzi katika viwanda vinavyozalisha na maduka yanayouza vyakula hivyo katika Mikoa ya Dar-es-salaam na Pwani kuanzia Novemba 30 hadi Desema mosi mwaka huu.

Amesema msako huo utaanza kwa wazalishaji wote wa vyakula vya mifugo hapa nchini ili kuzalisha vyakula vyenye uwiano sahihi wa viinilishe vinavyohitajika kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na Mamlaka ya Kuthibitisha Ubora wa Vyakula (TBS) na viwango vya kimataifa kwa wale watakaohitaji kusafirisha nje ya nchi.

“Lakini pia tunawaagiza kila kundi la chakula wanalozalisha wahakikishe sampuli yake inapelekwa kwenye maabara kuu ya veterinari ambao ndio wenye ithibati ya kitaifa ya kuchambua vyakula vya Mifugo ili waweze kuthibitisha na kutoa vyeti vya ubora,” amesema.

Vile vile amewataka wazalishaji kuhakikisha wanapima malighafi zote wanazotumia kutengeneza vyakula vya mifugo huku pia akiwaelekeza kusajili Taasisi na mahali wanapozalishia vyakula hivyo.

“Tunafahamu kwamba usajili ni kila mwaka hivyo wale ambao hawajasajiliwa wafanye hivyo na wale ambao tayari wameshasajiliwa waendelee kuhuisha usajili wao kupitia tovuti ya Wizara ambako watapata maelekezo yote ya kufanya mazoezi hayo,” amesema.

Amewataka wauzaji wa vyakula kununua vyakula vyao kutoka kwa wazalishaji waliothibitishwa kwenye viwango vya ubora kwa kila kundi la chakula wanalotaka kununua kwa wazalishaji hao.

Naye mzalishaji wa vyakula vya mifugo kutoka Pwani, Samson Maro amepongeza Serikali kwa kufanya msako huo, aliahidi kutekeleza aliyoelekezwa na wataalam.

Kwa upande wake muuzaji wa chanjo na Vyakula vya kuku na bata kutoka mkoani humo, Domitila Melisa ameeleza jinsi anavyosaidia wafugaji waliopo kwenye eneo lake kwa kuwapa elimu na ushauri kuhusu aina ya chakula wanachopaswa kupewa ndege kulingana na umri walionao.

Mfugaji wa kuku kutoka Kibaha mkoani Pwani, Mwajuma Mwami amesema alikuwa akinunua vifaranga na chakula cha kuku wake kwa kubahatisha jambo lililokuwa linasababisha vifo vya mara kwa mara vya vifaranga hao ambapo ameiomba Serikali kufanya zoezi la ukaguzi na uhakiki wa viwanda na maduka ya vyakula vya mifugo kuwa endelevu.

Uzalishaji wa vyakula vya mifugo nchini unasimamiwa na sheria ya Nyanda za malisho na chakula cha mifugo ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake zilizoandaliwa mwaka 2013,

Kwa pamoja vinawataka wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo kuhakikisha wanyama wanapata vyakula bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button