MSD yafunga mashine hospitali ya Msoga

Bohari ya Dawa (MSD) imefunga mashine za picha za mionzi (X-Ray mashine) ambazo zimeanza huduma katika Hospitali ya Msoga iliyopo Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani.

MSD imepeleka majokofu ya kisasa kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti, mashine ya usingizi, vitanda, magodoro na vifaa vingine vya kutolea huduma za kihospitali.

Akizungumza na waandishi wa habari mfamasia wa hospitali hiyo, Shaaban Kinesi amesema Kuanza kutolewa kwa huduma ya picha za mionzi (X-Ray) katika hospitali hiyo zinatoka haraka na zina uwezo wa kumfikia daktari mara moja.

Advertisement

Kwa upande mwingine wagonjwa wamepunguziwa adha ya kusafiri umbali mrefu ambao ni zaidi ya kilometa 80 kufuata huduma hiyo. Kabla ya huduma hizo katika hospitali hiyo, wagonjwa 15 hadi 20 walikuwa wanapewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoani Pwani.

“Hiyo ilikuwa inasababisha gharama na kupoteza muda mwingi kwa mgonjwa lakini MSD imetuletea huduma hizi zinapatikana katika hospitali ya Msoga,” alisema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, Mfamasia huyo alisema hali ya upatikanaji dawa unaridhisha kwani dawa zote muhimu kutoka MSD zinapatikana kutokana na kuzingatia vigezo wakati wa maombi.

Kwa upande wake, Ofisa Huduma kwa Wateja Kanda ya Dar es Salaam, Mfamasia Diana Kimario alisema mahitaji yote muhimu yanaendelea kupelekwa kuhakikisha huduma bora kutolewa kwa wananchi.