MSD yataja hatua saba kuimarika upatikanaji bidhaa za afya

DODOMA: MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya dawa (MSD)Mavere Tukai, ametaja hatua saba wanazoendelea kuchukuwa ili kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini ikiwemo mabadiliko ya muundo wa taasisi na maboresho ya maeneo ya uhifadhi wa bidhaa.

Tukai amesema hayo jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dodoma.

Amesema sababu zingine ni matumizi ya mifumo ya tehama, mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi na maboresho ya mikataba ya wazalishaji na washitiri.

Advertisement

“Mengine ni ongezeko la watumishi ili kukidhi mahitaji na uanzishaji wa kampuni tanzu kwa ajili ya kusimamia viwanda,”ameeleza.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameupongeza uongozi wa MSD kwa mabadiliko makubwa yanayoendelea katika taasisi ambayo kwa kiasi kikubwa yamewezesha kupunguza malalamiko ya uhaba wa bidhaa za afya nchini hasa uhaba wa dawa.

” Awali tukienda kwenye mikutano ya hadhara kuongea na wananchi, tulikumbana na malalamiko mengi ya uhaba wa dawa, lakini hivi karibuni hali imebadilika, japokuwa bado kuna changamoto, lakini angalau inatia moyo kuona kuna mageuzi yanafanyika.

Amesema Dk Samia Suluhu Hassan ameleta mapinduzi makubwa, katika kipindi kifupi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

“Tunapoongelea maboresho ya Sekta ya Afya na mabadiliko ya huduma hatuwezi kuacha kumtaja Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kama kiongozi mkuu aliyeongoza mapinduzi haya, kwani tumeshuhudia ongezeko kubwa la bajeti ya bidhaa za afya, miundombinu ya afya, ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la vifaa tiba katika ngazi zote za kutolea huduma kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa” amesema Senyamule